July 29, 2016


Na Saleh Ally
NINAJUA mfano huu wa kitambi unaweza kuwa kidogo haufanyi kazi kwa wale ambao hawajawahi kupata kitambi, hasa kile kinachotokana na kula au kunywa bila mpangilio.
Pia mfano unaweza kuwa mzuri na unaoeleweka sana kwa wale waliowahi kupata kitambi au wanacho kutokana na uzembe wa mazoezi au kula na kunywa bila ya mpangilio.

 Kitambi maarufu kama ‘mgeni’, kila aliyenacho mwanzoni huona ni kama sifa, kukua au ishara ya maisha bora kutoka katika umbo la wembamba ambalo kwa wengine au wengi huamini ni ishara ya shida.

Inapoanza adha ya kitambi, wengi huanza kugundua wameingia ‘chaka’, mara moja juhudi ya kuanza kuking’oa huanza na wengi wameshindwa na mwisho wake kuishia kusema; “wamechoka” na kitambi si ugonjwa.

Klabu za Ligi Kuu Bara, hasa zile kubwa au kongwe zimekuwa zikilalamika kuhusiana na mkataba wa TFF, Bodi ya Ligi na Azam TV kuhusiana na suala la wao kupungukiwa mapato kupita kiasi.

Ukiangalia, kuonekana kwa mechi moja kwa moja, kwa kiasi fulani kumechangia watu wengi kupungua kwenda uwanjani, hili linapunguza mapato ya mlangoni.

Hakuna anayeweza kukataa eti klabu zinakosea kutegemea mapato ya mlangoni na hata zile za Ulaya, zinategemea hilo na zimekuwa zikipandisha bei hadi inafikia mashabiki wanaamua kuandamana. Tumeliona hili hasa kwa klabu ya Arsenal.

Hapa Yanga na Simba ambazo zina mashabiki wengi, zimelalamika sana kuhusiana na kupata fedha sawa na klabu nyingine za Ligi Kuu Bara kwa kuwa ndizo zina mtaji mkubwa wa mashabiki.

Ninaungana nazo kwa kuwa zina mtaji wa mashabiki, ninaungana nazo kuwa ndizo zinafanya Ligi Kuu Bara kuwa maarufu na kufuatiliwa na hata ikawavutia Azam Media kuona inaweza kuingiza mabilioni ya fedha.

Tuwapongeze Azam Media kuingiza fedha nyingi kwenye ligi hiyo, lakini msisitizo ni kwamba bado kuna nafasi ya kuangalia Yanga na Simba zinafaidika zaidi pia kwa kuwa hilo halina ubishi hizi ni klabu zenye mtaji mkubwa wa mashabiki. Wadhamini, hufuata kwenye mashabiki wengi.

Wadhamini siku zote wao wanachotaka ni kuonekana tu. Kama watamwaga fedha zao, wanachoangalia ni kule bidhaa zao zitakapoonekana sana. Kwenye mashabiki wengi ndiyo sehemu mwafaka na Yanga na Simba, ndiyo wenye mtaji huo.

Wakati hilo likiendelea, si kweli kwamba Yanga na Simba sasa wanapaswa kulala na kusubiri tu hadi pale mambo yatakapobadilika yenyewe. Wanaweza kujifunza kwa urahisi kwa kuwa hata klabu kubwa kama Real Madrid, Barcelona, Manchester United, Bayern Munich, Juventus na nyingine, zimekuwa na kitengo bora na imara, kikubwa na chenye wabunifu.

Kinaweza kuwa kitengo cha masoko ambacho kitatafuta wadhamini zaidi ambao wakiingia, wangeweza kuzisaidia klabu hizo kuingiza fedha nyingine ambazo zingewasaidia kujikimu na kufanya vema zaidi kimaendeleo.

Mfano, huu ni wakati mzuri kitengo hicho kuanza kuitumia Azam TV kupata wadhamini wengi kwa kuwaambia, zamani walikuwa wakionekana uwanjani tu na sasa wanaonekana Tanzania nzima kila Simba au Yanga inapocheza kwa kuwa mechi zinaonekana Tanzania kote na hata nje ya Tanzania.

Hii inaweza kuwavuta zaidi wadhamini ambao wangependa kujitangaza. Waende katika mashirika mbalimbali yakiwemo hata yale ya kimataifa kupitia ubalozi wa nchi mbalimbali na kuwaeleza wanavyoweza kushiriki katika kampeni zao mbalimbali za kibinadamu na kusambaza ujumbe vizuri.

Jezi za Yanga na Simba zenye mtaji wa mashabiki, tofauti yake na jezi ya JKT, Mgambo ambazo ni timu za jeshi ni rangi tu. Lakini katika uhalisia, jezi hizo zilipaswa kutofautiana kwa wingi wa matangazo ambayo yanaingiza fedha.

Tumeona Ulaya, matangazo begani, mgongoni, kwenye paja na hata kwenye makalio. Yote yanaingiza fedha. Simba na Yanga wao vipi!1 COMMENTS:

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV