Huku akiendelea kukinoa kikosi chake kipya cha Simba, Kocha wa timu hiyo Mcameroon, Joseph Omog ameomba kucheza michezo mitatu ya kirafiki ya kimataifa sawa na dakika 270 kwa ajili ya kukipima kikosi hicho.
Timu hiyo, hivi sasa ipo Mkoani Morogoro kwa ajili ya kambi ya pamoja kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara chini ya Mcameroon huyo na Mganda, Jackson Mayanja.
Wakati akiendelea kukinoa kikosi chake, kocha huyo anaendelea na mchujo wa wachezaji wa kimataifa wanaokwenda mkoani humo kwa ajili ya majaribio.
Katibu Mkuu wa timu hiyo, Patrick Kahemele alisema yapo baadhi ya mapendekezo waliyoyapokea kutoka kwa kocha ikiwemo hilo la kucheza mechi tatu za kirafiki kabla ya kuanza kwa ligi kuu.
Kahemele alisema, kikubwa kocha anataka kuona sehemu zenye upungufu atakazoziimarisha kabla ya kuanza kwa ligi kuu na lengo ni kuwa na kikosi imara kitakacholeta ushindani ndani ya uwanja.
"Wakati kocha akiendelea na program ya fiziki huko Morogoro, tayari tumepokea baadhi ya mapendekezo muhimu ikiwemo la kuomba kucheza mechi tatu za kirafiki za kimataifa baada ya kumaliza program hiyo ya fiziki.
"Bado hatujajua tutacheza na timu gani, hivi sasa tupo kwenye mazungumzo na baadhi ya timu ambazo tusingependa kuzitaja hadi pale zitakapothibisha kucheza.
"Na hiyo imetokana na nchi hizi za Afrika kutofautiana vipindi vya maandalizi ya ligi kuu, zipo nyingine ligi zao zimemalizika na nyingine ambazo zipo kwenye usajili, hivyo hali hiyo inatupa ugumu kama uongozi, lakini kila kitu tutakiweka wazi hivi karibuni,"alisema Kahemele.
0 COMMENTS:
Post a Comment