July 30, 2016Na Saleh Ally
MFANYABIASHARA maarufu nchini Mohammed Dewji maarufu kama Mo, ametangaza nia yake ya kutaka kuinunua klabu maarufu nchini ya Simba.

Uamuzi wake unashereheshwa na maamuzi ya kuweka Sh bilioni 20, halafu akatiwe kipande cha asilimia 51 ya umiliki wa Simba na 49 zilizobaki ziwe mali ya wanachama wa klabu hiyo.

Maana yake, Simba itamilikiwa na Mo, pamoja na wanachama wengine wa klabu hiyo ambao watamiliki hisa hizo. Nianze kwa kusema, hili ni wazo zuri kabisa ambalo Simba, hata wafanyeje hawatalikwepa, badala yake ni muda tu.

Lakini ninaweza kuhoji, kwamba pamoja na uzuri wa kulifikiria hilo kama jambo bora, lazima Simba wawe makini na wapige hatua kwa uhakika kuingia kwenye mchakato huo hadi kufikia mabadiliko badala ya kukurupuka na kutaka kufanya mambo kwa kishabiki.

Mo amezungumza mambo kadhaa ambayo yana mashiko. Nami ningependa kukazia kwa ubora wake au kuhoji kupitia udhaifu niliouona.

Wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Mo alisema anayepinga uamuzi wake huo atakuwa si mpenda maendeleo ya Simba, lakini naona ni vizuri kila atakayekuwa tayari kuingia kwenye mabadiliko, basi asihofie kuonekana amepinga na badala yake ahoji ili kuingia kwa uhakika upande wa pili.

Moja:
Mo amesema bajeti ya Simba kwa mwaka ni Sh milioni 500 hadi 700 hivi, wakati Azam FC na Yanga wana bajeti ya hadi Sh bilioni 2.5, jambo ambalo anaamini kweli Simba haiwezi kushindana na wapinzani wake.

Mimi: Ninachoona, Simba lazima iainishe kama kweli suala la bajeti hiyo ya Sh bilioni 4 kwa mwaka linawezekana, lazima kuwe na mchanganuo sahihi kwamba fedha hizo zitatoka wapi, mfano kwa wadhamini au mwekezaji pekee na nani atatoa kiasi gani.

Mo pia amesema kama ni bajeti ya Sh bilioni 4, basi itabaki Sh bilioni 1.5 ambayo itatumika kujenga uwanja, gym, hosteli na kadhalika. Hili ni jambo zuri, lakini kama tena Simba itabaki na bajeti hiyo ya Sh bilioni 2.5 baada ya kukata hiyo bilioni 1.5, itakuwa kwenye njia sahihi ya kuzipiku Yanga na Azam FC?

Mbili:
Mo amesema Sh bilioni 1.5 kama zitatumika kujenga uwanja. Hili ni jambo jema tena ambalo Wanasimba wanaweza kulifurahia ingawa taarifa zinaeleza tayari wameshaanza kazi ya ujenzi.

Mimi: Kama fedha hizo zitatumika kujenga uwanja, vizuri pia kila kitu kiwekwe wazi ni muda gani utakuwa umeisha, ni uwanja wa aina ipi na uwezo upi na utaisaidiaje Simba kuingiza mapato kama chanzo na kwa mwaka unaweza kusaidia kuzalisha kisi gani?

Tatu:
Mo amezungumzia hisa za bure kwa wanachama. Kwamba baada ya yeye kununua hisa asilimia 51 kwa Sh bilioni 20, wanachama wengine wa Simba watapewa hisa zilizobaki bure hasa wanachama wa zamani na atashirikiana na uongozi.

Mimi: Neno kushirikiana na uongozi uliopo ni neema nyingine ila ni vizuri kabla ya wanachama hao kupewa hisa hizo bure, basi waelimishwe kwanza na kujua nini maana ya hisa na thamani yake na wajue kuziuza ni kujiondoa kwenye umiliki wa klabu, faida na hasara zake.

Hata kama wapo wanaoficha, lakini ukweli asilimia 95 ya mashabiki na wanachama wa klabu hiyo hawajui lolote kuhusiana na maana ya hisa. Kuwaburuza ni kuwaonea, hivyo elimu iwe kwanza, suala la kuwapa bure linaweza kufuatia na huenda litakuwa kwenye ubora zaidi baada ya watu kupigwa ‘brush’ kielimu.

Nne:
Mo alisema hivi; zile Sh bilioni 20 hazitaguswa na mtu, badala yake zitapelekwa kuikopesha serikali. Kila mwaka Simba itakuwa ikipata faida ya Sh bilioni 3.5 au 7.5 baada ya miaka mitano. Kama ni hivyo ni jambo bora kwa kuwa Simba itaingiza zaidi wakati fedha zake zitaendelea kuwepo na inaingiza faida.

Mimi: Ambacho ufafanuzi bado haujatolewa zaidi katika Simba ni hizo Sh bilioni 20, kama ndiyo zimetolewa kuinunua Simba, halafu zinapelekwa mkopo serikalini. Je, Simba itaweza kujiendesha na fedha ya faida pekee? Swali jingine, Mo katoa Sh bilioni 20 kuimiliki Simba, zile fedha ni za nani? Vipi hawapewi wenyewe na kama hawapo wako wapi?

Maana zinawekwa benki, kama ni hivyo faida yake ikitumika kuiendesha Simba ambayo inamilikiwa kwa asilimia 51 na Mo, hauoni hii inampa faida yeye tena. Na je, atakuwa na umiliki wa fedha hizo baada ya kuzitumia kuinunua Simba!

Ambacho hakieleweki vizuri ni hivi, kama Mo ataimiliki Simba kwa asilimia 51, yale majengo ya Msimbazi na mali nyingine za Simba ni mali yake kwa asilimia 51. Fedha hizo zikiendelea kubaki kuwa za Wanasimba wote akiwemo yeye, maana yake atakuwa anazimiliki hizo Sh bilioni 20 kwa asilimia 51 pia?

Ndiyo maana ninasisitiza kuwa jambo hili ni zuri sana ila Wanasimba wanapaswa kwenda nalo kwa kukubali kujifunza, walielewe ili wakiingia kwenye mchakato na mwisho kupata jibu, wasiwe wanaelea kwa kushindwa kujua njia waliyopitia kufika walipo.

Hii maana yake, Simba watakwenda na kila kitu pamoja bila kuacha maswali mengi nyumba yao na hawatakuwa na sababu ya kujilaumu hapo baadaye.

1 COMMENTS:

  1. jembe siku hizi hatuhangaiki sana kuujua msimamo wa kassim dewji na wenzake,tukikusoma wewe tu tunajua ndicho anachokiamini kassim na kikundi chake,umekubali kuwa kasuku wake?

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV