July 2, 2016


Wakati leo anapanda 'kizimbani', Jerry Muro amesema wazi kuwa leo ataenda katika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pale Ilala jijini Dar es Salaam kuitikia wito wa kwenda kuhojiwa na Kamati ya Nidhamu lakini anajua kuna mpango wa kufungiwa miaka mitatu.

Muro ambaye ni ofisa habari wa Yanga, amesema kuwa, kuna mpango umesukwa ili afungiwe na amejiandaa na hatokubali kuona anaonewa.

TFF kupitia katibu mkuu wake, Selestine Mwesigwa, Jumatano wiki hii ilimuandikia barua Muro ili aende kuhojiwa na Kamati ya Nidhamu kutokana na kauli zake dhidi ya shirikisho hilo.

“Mimi nitafika TFF kesho (leo) kwa muda niliopangiwa mapema, lakini nahitaji kabla sijafika waniombe radhi kufuatia kuninyima haki yangu ya msingi na nawaambia mapema kwamba safari hii maiti itamng’ang’ania mwoshaji.

 “Nitazungumza yale niliyokubaliana na uongozi wangu, kwanza mimi ni muajiriwa wa Yanga lakini nashangaa barua imekuja moja kwa moja kwangu bila ya kupitia kwa katibu.
“Barua itakujaje kwangu moja kwa moja wakati mimi siyo mwanachama wa TFF, Yanga ndiyo mwanachama wa TFF, lakini ngoja tuone itakavyokuwa.

 “Nimesikia wanataka kunifungia kwa muda wa miaka mitatu, ngoja tuone ninachotuhumiwa nami nitawajibu hakuna tatizo,” alisema Muro.


Muro alisema Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Mwesigwa wamemdhalilisha kutokana na jambo hilo kwa kuwa yeye ameajiriwa na Yanga, hivyo hawezi kusema lolote bila ya kuagizwa na viongozi wake.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV