Wachezaji wa Yanga wameipongeza ratiba ya Ligi Kuu Bara msimu ujao ambayo imetolewa hivi karibuni na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ila wameenda mbali kidogo kwa kusema; “Kwa jinsi tunavyoiona basi ubingwa ni wetu tena.”
Wamedai kuwa watani zao Simba na Azam FC wajipange kuwania ubingwa wa Kombe la FA ili waweze kupata tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa lakini kuhusu ubingwa wa ligi kuu wasahau.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, ligi kuu itaanza Agosti 20, mwaka huu ikitanguliwa na mchezo wa Ngao ya Jamii Agosti 17, kati ya Yanga na Azam.
Kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima alisema: “Nimeiona ratiba hiyo, ni nzuri kwa kiasi chake ukilinganisha na ile iliyopita, ni matumaini yangu tunaweza kutetea ubingwa wetu kama TFF wasipoivuruga.”
Kwa upande wake, Amissi Tambwe alisema: “Ratiba nimeiona na imepangwa vizuri kwani zaidi ya mechi zetu tano za mwisho tutacheza kwenye uwanja wetu wa nyumbani.”
“Msimu uliopita idadi ya mechi kama hizo tulicheza ugenini tena mfululizo bila ya kupumzika, endapo Mungu atakuwa nasi na ratiba isipovurugwa, tutatetea tena ubingwa wetu,” alisema Tambwe.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment