July 20, 2016


Kikosi cha Yanga kinatarajia kuondoka nchini keshokutwa Ijumaa kuwafuata Medeama ya Ghana tayari kwa mchezo wa marudiano wa kuwania Kombe la Shirikisho Afrika.

Hata hivyo, katika safari hiyo beki wa kulia wa Yanga aliyejiunga na timu hiyo hivi karibuni akitokea Simba, Hassan Kessy, anaweza kuikosa mechi hiyo kutokana na sakata lake la usajili linaloendelea hivi sasa kati yake na Simba.

Habari za kuaminika kutoka Yanga zimedai kuwa maandalizi kwa ajili ya safari hiyo yanaendelea lakini pia kocha mkuu wa timu hiyo, Mholanzi, Hans van Der Pluijm yupo katika maandalizi makali kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa siku ya Jumanne ijayo, Julai 26, mwaka huu.

“Tupo katika maandalizi makali kwa ajili ya mechi yetu ya marudiano na Medeama itakayofanyika Jumanne ijayo ili kuhakikisha tunafanya vizuri kwani nafasi tuliyopo hivi sasa inatunyima usingizi.

“Mungu akipenda kama mambo yatakuwa sawa tutaondoka Ijumaa hii ila wachezaji ambao hawatacheza mechi hiyo kutokana na kuwa na adhabu mbalimbali na wale ambao hawajapata kibali cha kuitumikia Yanga basi tunaweza kuwaacha lakini tunasubiria mapendekezo ya kocha,” alisema mtoa habari huyo.

Alipoulizwa kuhusiana na suala hilo Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deustedit hakuwa tayari kulizungumzia zaidi ya kudai kuwa: “Muda ukifika kila kitu kitajulikana.”
Yanga itakwenda nchini Ghana ikiwa na kumbukumbu ya kutoshana nguvu ya kufungana bao 1-1 na Medeama Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga kwa sasa inashika mkia kwenye Kundi A ikiwa na pointi moja huku TP Mazembe wakiwa kinara na pointi saba, wakifuatiwa na MO Bejaia wenye pointi tano.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic