August 15, 2016


Huku Yanga ikijiandaa kutupa karata yake ya mwisho katika mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo, ghafla imejikuta ikipokea taarifa mbaya na nzuri kwa wakati mmoja.

Taarifa nzuri ni kwamba mshambuliaji wao hatari, Mzimbabwe, Donald Ngoma waliyemkosa katika mchezo uliopita dhidi ya MO Bejaia ya Algeria, amemaliza adhabu yake ya kadi mbili za njano na atakuwemo katika mechi ya Mazembe.

Lakini wakati huohuo, beki kisiki wa Yanga, Kelvin Yondani ataikosa mechi hiyo ya Mazembe itakayopigwa Agosti 23 jijini Lubumbashi, DR Congo kutokana na kuwa na adhabu ya kadi mbili za njano.

Yondani alipata kadi ya pili ya njano katika mchezo wao wa juzi walioumana na MO Bejaia na kuibuka na ushindi wa mabao 1-0. Kabla ya mchezo huo tayari Yondani alikuwa na kadi moja ya njano.

Yondani ambaye aliingia dakika ya 16 kuchukua nafasi ya Andrew Vincent ‘Dante’, alipata kadi hiyo katika dakika ya 74. Dante alimpisha Yondani baada ya kupata majeraha kwenye msuli wa paja.

Pamoja na hayo, Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, ameeleza kwamba kwa hatua waliyofikia kwenye kombe hilo, wanapaswa kukubaliana na kupambana na kila changamoto inayowakuta, kama hii ya kuwakosa wachezaji wao muhimu kutokana na adhabu za kadi.

“Hatua tuliyopo ni kubwa na tunapaswa kupambana zaidi, hizi changamoto tunazokutana nazo lazima ziwepo na lazima tukabiliane nazo na kwa kuwa tunarejea kwenye maandalizi ya mchezo unaofuata, tutaangalia nini cha kufanya, mambo yatakaa sawa,” alisema Pluijm.

Yanga itacheza na Mazembe Agosti 23 katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi. Inahitaji ushindi ili angalau ipate matumaini ya kusonga mbele.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic