August 13, 2016


BUKUNGU (WA PILI KULIA MSITARI WA MBELE) AKIWA NA KIKOSI KIPYA CHA SIMBA.
Beki mpya wa kimataifa wa Simba, raia wa DR Congo, Janvier Bokungu, tayari ameshagundua kuwa kuna baadhi ya wapenzi wa soka hapa nchini wanamuona kuwa ni mchezaji wa kawaida sana ukilinganisha na wengine waliosajiliwa na timu hiyo msimu huu.

Kutokana na hali hiyo, Bokungu amedai kuwa hao wanaomuona hivyo, ipo siku watampenda tu kutokana na kazi kubwa atakayokuwa akiifanya uwanjani.

Bokungu alisema kuwa yeye siyo mchezaji wa kucheza na majukwaa, isipokuwa anapokuwa uwanjani hucheza kwa kuzingatia maagizo ya kocha wake.

“Inawezekana kabisa, ndiyo maana wananiona kuwa ni mchezaji wa kawaida lakini naamini kabisa kuwa ipo siku watanikubali tu kwani hivi sasa najifua vilivyo ili niweze kurejea katika kiwango changu cha siku zote kwa sababu kabla ya kuja Simba nilikuwa nimepumzika kwa muda mrefu bila ya mazoezi.


“Hata hivyo, naomba watu hao wajue mimi nimekuja Simba kwa kazi moja tu ya kucheza soka na nitahakikisha naifanya kazi kwa nguvu zangu zote, naomba Mungu anisaidie kwa hilo,” alisema Bokungu ambaye pia ana uwezo wa kucheza uwanjani nafasi zote za ulinzi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV