August 13, 2016


Baada ya kuamini kwamba ana kikosi imara, Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, ametangaza vita kwa makocha wa timu za Yanga, Hans van Der Pluijm na Azam FC, Zeben Hernandez kwa kusema kuwa lazima ashiriki michuano ya kimataifa mwakani kwa kutwaa ubingwa msimu ujao.

Ligi Kuu Bara inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 20 ambapo Simba itafungua dimba dhidi ya Ndanda FC katika Uwanja wa Taifa jijini Dar ambapo matarajio ya wengi ni kuona timu hiyo itafanya nini katika mchezo huo.

Simba haijashiriki mashindano ya kimataifa takribani misimu minne mfululizo, hivyo imeamua kufanya usajili wa nguvu utakaoleta ushindani msimu ujao.

Omog amefunguka kuwa anahitaji kufanya vyema kwenye ligi ili aweze kushiriki michuano ya kimataifa kwa kuhakikisha anatwaa ubingwa.

“Maandalizi ya ligi yanakwenda vizuri na kila mchezaji anaonyesha kujituma ipasavyo mazoezini lakini bado nahitaji kila mmoja aonyeshe uwezo na kujituma.


“Tunajiandaa vizuri na ligi na tunasubiri itakapoanza, nahitaji kushiriki michuano ya kimataifa mwakani kwa kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye ligi kwa kutwaa ubingwa, kikosi changu kipo vizuri na wachezaji wote kwangu ni wazuri,” alisema Omog.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV