August 12, 2016

HAJI MWINYI

Kocha Mkuu wa Yanga, Mdachi, Hans van Der Pluijm, ameamua kufunguka kilichopo nyuma ya pazia kuhusiana na shutuma na malalamiko yanayomwandama beki wa kushoto wa timu hiyo, Haji Mwinyi kuwa anaporomoka kiwango kila kukicha kwa kuwa hana nidhamu ya kanuni za soka kwa sasa.

Mwinyi aliyetua Yanga mwanzoni mwa msimu uliopita akitokea KMKM ya Zanzibar, awali alikuwa kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo kutokana na uwezo aliokuwa akiuonyesha lakini katika mechi za hivi karibuni, hasa za michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, amekuwa akilalamikiwa na mashabiki wa Jangwani kuwa kiwango anachoonyesha kimeshuka.

PLUIJM

Pluijm amesema kuwa wengi wanashindwa kuelewa kuwa Mwinyi alitumika muda mrefu na kwamba hivi karibuni amerejea kutoka kwenye majeraha, hivyo alihitaji muda na sasa ameanza kurejea kwenye kiwango chake stahiki.

“Hapana, nafikiri kinachozungumzwa siyo sawa, Mwinyi hajashuka kiwango, ieleweke kwamba kijana ametumika muda mrefu na baadaye akawa majeruhi lakini kwa sasa ndiyo kwanza anarudi, hata kwenye mechi ya mwisho ya kirafiki na Mtibwa Sugar alicheza vizuri.


“Bado naendelea kumwangalia katika mazoezi tunayoendelea kufanya kwa ajili ya MO Bejaia, akiwa fiti zaidi kwa ajili ya mchezo naweza kumtumia,” alisema Pluijm aliyeiongoza Yanga kutwaa ubingwa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo sasa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV