August 14, 2016


Na Saleh Ally
BAADA ya ushindi wa juzi, Yanga ilirudisha matumaini ya kufuzu kwenda kucheza hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho baada ya kuandika ushindi wa kwanza.

Yanga imeifunga Mo Beijaia kwa bao 1-0 na kuwa ushindi wake wa kwanza baada ya kuwa imepoteza mechi tatu na kupata sare moja tu nyumbani dhidi ya Medeama ya Ghana.

Yanga ililazimika kusubiri tena matokeo ya jana wakati TP Mazembe ikiivaa Medeama ugenini. Yanga iliomba Waghana hao wakiwa nyumbani wapoteze ili iendelee kufufua matumaini yao zaidi.

Tuyaache hayo ya matumaini ya Yanga, ukweli ni kwamba wakati Yanga ikishiriki michuano hiyo hatua ya makundi haikuwa na ushirikiano mzuri kutoka kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Nimeamua kulikumbushia hili kwa kuwa binafsi ninaamini bado Yanga ina nafasi ya kujifunza hadi kufikia katika hatua makundi, kwa timu za Tanzania imekuwa muda mrefu sasa.

Pamoja na hivyo, shirikisho linapokuwa karibu na timu yake ni sawa na mzazi na mtoto kuwa pamoja kugombea kuwania jambo fulani, lazima watafanikiwa.

Kufanikiwa kungetokana na picha ya umoja ambayo matunda yake huwa ni ushindi, lakini TFF haikuwa tayari kuisaidia Yanga, ilikuwa ni kama TFF nayo ni sehemu ya timu za Kundi A katika Kombe la Shirikisho.

TFF ilionyesha kukasirishwa na Yanga kugusa maslahi yake, suala la kuingiza mashabiki bure. Kwanza hii inaonyesha namna ambavyo viongozi wake hawakuwa na busara, maana ilionekana ni mashindano ya maslahi ya watu binafsi badala ya Utanzania.

TFF haikujali tena kama kuna Utanzania. Badala yake ikaangalia suala la kukosa fedha na ushindani dhidi ya Yanga ukaanza. Huu ulichangia malumbano ya bila sababu tena kwa kipindi kirefu kabisa.

Yanga walikuwa kama vile wanashindana na mzazi wao wakati wanapambana na familia ya jirani. TFF haikuangalia kwamba kinachofanyika mbele yao ni mafanikio yao pia. Kwani kama Yanga ikifika nusu fainali, basi ni nafasi yao ya kufanya vizuri zaidi.

Viongozi wa TFF, wamekuwa hawataki kuambiwa walishindana na Yanga. Kama wakielezwa hili, huona kama wanaonewa lakini hii ni hali halisi, shirikisho hilo halikuangalia suala hili kwa jicho la tatu kwamba zaidi ni utaifa kuliko maslahi.

Sasa Yanga imefikisha pointi nne, lakini ingeweza kushinda mechi dhidi ya TP Mazembe au Medeama ingekuwa na pointi saba na tayari ingekuwa sehemu ya mshindani mwenye nafasi ya kufuzu.

Ninaposema kushirikiana, unajua ninamaanisha ukaribu wa kila kitu katika kujipanga na mengineyo kati ya shirikisho na klabu. Soka si uwanjani pekee, kuna maandalizi kabla ya hapo.

TFF ingeweza kuwa karibu na Yanga, lakini ilikerwa na jambo la fedha. Huenda kuna baadhi wangefurahi kuona Yanga haifanyi vema ili iumie kabisa, jambo ambalo naona pia si sawa.

Kokote kuna suala la kanuni, lakini katika kusigana pia kuna suala la busara. Katika maisha ya kawaida, hili haliwezi kukwepeka, wote tunajua.

Ukiangalia vita ya TFF na Yanga, zaidi ni sawa na kusema vigogo wawili wanaotaka kuonyeshana mabavu. Huyu anataka kuonyesha ni jeuri na huyu anaweza, basi mwisho inaumia klabu na Watanzania.

Lakini inakosa nafasi ya kusonga mbele kwa kuwa nafsi mbili au tatu zinataka kuonyesha ubabe. Hili si jambo sahihi na vema likawa ni funzo kwa kuwa Yanga inaendelea kushiriki michuano ya kimataifa.


TFF lazima ikubali, inahusika katika kusaidia ushiriki wa klabu za Tanzania. TFF ni mali ya umma, tena umma wa Watanzania. Yanga ni timu inayotokea Tanzania. Tuache ubinafsi na kuonyeshana ubabe huku tukiliathili taifa letu. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV