August 15, 2016

SIMBA

Kasi iliyonayo Simba ya Mcameroon, Joseph Omog na maandalizi makali ya Azam FC chini ya Mhispania, Zeben Hernandez, vimemtia kiwewe Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm kuelekea ufunguzi wa Ligi Kuu Bara mwishoni mwa juma hili.

Pluijm ambaye anasaka rekodi ya kuchukua ubingwa huo kwa msimu wa tatu mfululizo, tayari ameeleza hofu yake kuwa anatakiwa kuwa makini kutokana na kikosi chake kukosa muda wa kupumzika kulinganisha na wapinzani wake.

Simba yenye sura mpya nyingi, imeonyesha kuwa fiti kama ilivyo Azam ya Mhispania kutokana na timu zote kupata muda wa kupumzika na kujiandaa vema wakati Yanga haijapumzika kutokana na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

PLUIJM

“Kweli ligi inaanza lakini hatuna maandalizi ya kutosha kwa kweli. Tulikuwa bize na Caf, wachezaji hawajapumzika, hivyo lazima tuchukue tahadhari kubwa na ligi. Sitaki niwatumikishe sana wachezaji wangu, lakini yote kwa yote nisema hii (michuano ya kimataifa) siyo maandalizi mazuri kwa ajili ya ligi kuu.

“Wenzetu (wapinzani) walipata nafasi ya kupumzika. Natarajia watakuwa na faida ya ziada,” alisema kocha huyo wa zamani wa klabu za Medeama na Berekum Chelsea za Ghana.

Simba ndiyo timu ambayo inatazamwa kama imejiandaa zaidi kwa ajili ya ligi kutokana na kufanya usajili mzuri na kuwa kwenye kiwango bora katika mechi zake kadhaa za kirafiki.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV