August 17, 2016


Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Yanga, Mzee Ibrahim Akilimali, amemuomba radhi mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji, baada ya kutoa kauli yake kwamba Manji amekurupuka kufuatia kutaka kuikodisha Yanga kwa muda wa miaka kumi na kudai kuwa hakudhani kwamba ingetafsiriwa vibaya.

Hivi karibuni, Mzee Akilimali alisikika kwenye vyombo vya habari akimponda mwenyekiti huyo kuwa amekurupuka kufuatia madai yake ya kutaka kuikodisha Yanga, jambo ambalo limezua kizaazaa na kusababisha taarifa kuzagaa kuwa mwenyekiti huyo anataka kujiuzulu.

Akizungumza jijini Dar, Akilimali alisema kuwa, amemuomba radhi Manji kufuatia kauli yake aliyoitoa pamoja na kuwaomba msamaha Wanayanga wote kuwa alitamka neno hilo bila ya kujua kama linaweza kuleta madhara na kudai kuwa neno kukurupuka siyo tusi na kueleza kuwa bado wanahitaji kuwa na mwenyekiti huyo.

“Mimi nimethubutu kuzungumza na Manji kwa kinywa chake na kumueleza kuwa kama neno kukurupuka ni tusi, basi namuomba radhi mwanangu kwani nilichokuwa nikizungumza kwenye vyombo vya habari ni kwenda kinyume na utaratibu wa siku zote tuliouzoea, ndiyo maana nilimwambia vile.

“Nimeshtuka sana baada ya kusikia kuwa Manji amejiuzulu kwani ukitazama mimi nimempa ngao na vyeo vingi lakini nilichokuwa nikijaribu ni kuweka sawa na kwenda na utaratibu wetu tuliouzoea wa kukutana na Baraza la Wazee ili atueleze dhamira yake na atuheshimu kama wazee ili tuweze kumwambia aendelee.


“Nampenda sana Manji kwani ametutoa mbali sana, nimemuomba radhi pamoja na Watanzania na wanachama wote, bado tunamtaka lakini mimi nilikuwa nikifanya vile kwa kuwa tulikuwa tunataka aendelee kama ilivyokuwa huko nyuma alivyokuwa akiisaidia timu, naomba radhi Watanzania wote kama nimekosea kusema neno hilo,” alisema Akilimali.

1 COMMENTS:

  1. Tatizo kubwa lililopo Tanzania ni utaratibu tuliuzoea huo ni ujinga wa mwisho katika kutafuta maendeleo je hilo kundi la wazee na kiongozi wao Akilimali linatoa mchango wa asilimia ngapi katika kuindesha klabu ya yanga kila siku, wiki,mwezi na mwaka au kwa kifupi katika bajeti ya klabu yao ambayo inakuwa siku hadi siku mchango wao ni kiasi gani au katika kuchonga mdomo tu na kujipaka sifa za wazee wa klabu? Kuendesha timu ni gharama kubwa tena sana bila ya nguzo imara za uchumi timu haiwezi hata kulipa mishahara ya wachezaji achilia mbali huduma nyengine za kila siku sasa Akilimali na wenzake mchango wao ni upi katika klabu yao?

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV