August 15, 2016


Kiungo mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya, ameweka bayana kuwa amejipanga kuonyesha uwezo wake wote ili kuipa ubingwa Simba msimu ujao, kisha baada ya hapo apate soko la kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Kichuya anayetumia jezi namba 25 ndani ya Simba, amejiunga na kikosi hicho kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro na tayari ameshaanza kuwa kipenzi cha mashabiki, baada ya kucheza kwa kiwango cha juu kwenye Tamasha la Simba Day, Jumatatu iliyopita.

Kichuya alisema kuwa kwa msimu huu amejipanga kuonyesha uwezo zaidi ya alipokuwa Mtibwa Sugar kwa ajili ya kuzivutia timu za nje ya Tanzania kumsajili kama ambavyo Simba ilivyovutiwa na uwezo wake.
“Hapa Simba wala sina mawazo ya kukaa kwa muda mrefu kwa sababu safari yangu ya kisoka sitaki iishie hapa kwa kuwa nina ndoto ya kwenda nje kucheza soka la kulipwa, hivyo Simba ni daraja langu la kufikia kule ninapotaka kwenda.


“Kwa ajili ya kulitimiza hilo nimejipanga kuonyesha uwezo mkubwa zaidi ya ule nilipokuwa Mtibwa pamoja na kuipa mafanikio timu yangu hii,” alisema Kichuya ambaye ameifungia Simba mabao mawili katika mechi mbili za kirafiki alizocheza.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV