August 15, 2016



Na Saleh Ally
BAADA ya mechi ya kirafiki dhidi ya AFC Leopards ya Kenya, mashabiki wa Simba wameonyesha kuamsha matumaini yao upya kuhusiana na kikosi chao kipya.

Simba iliitandika AFC Leopards kwa mabao 4-0 Jumatatu iliyopita katika mechi ya utambulisho wa wachezaji ambayo hufanyika kwenye tamasha maarufu la Simba Day.

Kama ilivyo kawaida ya mashabiki wa Simba, hata kama timu yao ishinde mabao mangapi, wanachotaka ni kuona soka la kitabuni linatandazwa. Kikosi hicho, kilionyesha uwezo katika hilo, ikawa furaha kuu.

Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali alikuwa uwanjani, alifanya kazi ya kuwalisha keki wadau mbalimbali. Alipata heshima hiyo kwa mengi, moja ikiwa ni ile ya yeye kuwa mwanzilishi wa tamasha la Simba Day.

Dalali, maarufu kama Field Marshal, alikuwa kati ya walioishuhudia timu hiyo ikionyesha umahiri kwa kucheza soka safi na kuwatundika wakongwe hao wa Kenya kwa mabao 4-0.


 Katika mahojiano maalum na SALEHJEMBE, Dalali anaungana na wale waliofurahia ubora wa kikosi hicho na kusema hata yeye ulimfurahisha. Lakini haamini uchezaji bora wa siku moja ndiyo kila kitu.

Dalali anaamini kuna mengi sana ya kufanya kuhakikisha Simba inakwenda vizuri hadi mwisho wa ligi na kufanikiwa kubeba ubingwa.

SALEHJEMBE: Unasema umefurahishwa na kikosi kama wengine, sasa una uhakika wa ubingwa?
Dalali: Ubingwa ni safari ndefu sana, kuna mengi yanapita hapo katikati, hivyo tufurahi lakini lazima tuwe na tahadhari.

SALEHJEMBE: Safari ndefu kivipi?
Dalali: Unajua tumeona mechi moja, lakini ligi ni mechi nyingi sana. Kuna mambo mengi tunatakiwa kufanya ndani ya Simba, pia mengine ni nje ya Simba.

SALEHJEMBE:Tufafanulie hayo ndani ya Simba, pia nje.
Dalali: Ndani ya Simba ni suala la umoja na ushirikiano. Lazima kuwe na upendo na si masuala ya wachezaji kuchukiana au wachezaji kutokuwa na uhusiano mzuri na benchi la ufundi. Umoja kama ilivyo kauli mbiu ya Simba ndiyo utakuwa msaada namba moja.


SALEHJEMBE: Kwani una hofu kwa sasa hakuna umoja?
Dalali: Ninajua haya mambo hutokea sana. Sasa nina uzoefu mkubwa, mnaweza kuanza vizuri na mwisho mkajiangusha wenyewe. Viongozi, wachezaji, benchi la ufundi wakiwa pamoja, hakuna anayeweza kuwaangusha.

SALEHJEMBE: Kuhusiana na nje ya Simba?
Dalali: Hapa sasa utahusisha haki na uadilifu. Mfano, suala la ratiba, unaweza kupangiwa kucheza Songea, ukirejea Dar, mechi inayofuatia ni Bukoba kucheza na Kagera Sugar. Hata uwe na wachezaji wazuri namna gani, watachoka na watashindwa kufanya vizuri. Hii pia inahusisha upangaji wa ratiba na kupangua, jambo ambalo TFF wanapaswa kuwa nalo makini ili kuepusha hisia za fulani anapendelewa na fulani anaonewa.

SALEHJEMBE:Umemuona Laudit Mavugo, mlitafuta kwa siku nyingi sana. Sasa mnaye, unafikiri tatizo la mabao litaisha kabisa?
Dalali: Kweli kijana ni mzuri, lakini bado tumpe muda. Haijui vizuri Tanzania, unajua ni kubwa kuliko Burundi, safari zake ni ndefu na anahitaji kuzoea mazingira. Sasa ikifikia siku moja kacheza chini ya kiwango, siyo watu waanze kumzomea.


SALEHJEMBE: Kama kacheza vibaya, wewe unataka mashabiki waendelee kushangilia tu, inawezekana?
Dalali: Mkude aling’ara kwenye Simba Day, naweza kusema ndiye Man Of The Match. Siku nyingine anaweza asiwe katika kiwango hicho, sasa wamzomee? Angalia Ulaya, timu imefungwa, watu wanaendelea kushangilia kwa nguvu hadi inasawazisha. Hapa mechi haijaisha, wapinzani wanaongoza, mashabiki wenu wanaanza kuzomea wachezaji wenu, hapa wanamsaidia adui na hamtasawazisha. Hili si sahihi, tujifunze.

SALEHJEMBE: Vipi kuhusu waamuzi?
Dalali: Hakika wao wanapaswa kuisaidia Simba, waisaidie si kwa kuipendelea, wafanye hivyo kwa kuchezesha haki. Maana msaada wao mkubwa ni kufanya mambo kwa haki wakifuata sheria 17. Kama watapindisha kwa makusudi kwa ajili ya kuwabeba wengine, watakuwa wanaiumiza bila sababu za msingi. Hata kama kuna mwamuzi ni shabiki wa Simba, yeye achezeshe haki tu ili tujipime na kujua maandalizi au usajili wetu ni sahihi au la na wapi pa kurekebisha.

SALEHJEMBE: Unaionaje ligi kwa jinsi timu zilivyo na nafasi ya Simba?
Dalali: Ligi Bara huwa ni ngumu kila msimu, mnatakiwa kushinda au kufanya vizuri kila mechi. Angalia Coastal Union, ndiyo timu iliyovifunga vigogo vyote, lakini ikateremka daraja, jiulize!

SALEHJEMBE: Nafasi ya Simba kama kikosi chenyewe ndani ya hayo matatizo uliyosema unaionaje?
Dalali: Nafasi ipo, tena nzuri kabisa, lakini haya niliyoeleza nayo ni muhimu sana. Wayafanyie kazi.

SALEHJEMBE: Kwa viongozi, unafikiri kipi wanatakiwa kufanya?
Dalali: Kikubwa ni umoja, angalia leo mzee Kilomoni alikuwa hauungi mkono uongozi huu, kwenye Simba Day tulikuwa pamoja. Simba wakae na wale Ukawa, wafute kesi mahakamani, wawarudishe uanachama na baada ya hapo, Simba iwe moja kama ilivyo kauli mbiu yetu ya Simba Nguvu Moja. Hakuna kitakachofanyika kwa ufasaha kama hakuna umoja.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic