Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm, raia wa Uholanzi, amesema kikosi chake kipo kwenye hali nzuri kuelekea mchezo wao wa Jumamosi hii dhidi ya MO Bejaia ya Algeria na tayari wageni hao wametua kwa siri.
Yanga inatarajia kucheza na MO Bejaia katika Uwanja wa Taifa, Dar ukiwa ni mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo huo utakuwa ni mchezo wa tano kwa timu hizo zilizopo Kundi A.
Yanga ambayo mpaka sasa haijaonja ladha ya ushindi kwenye mechi zake za hatua hiyo zaidi ya sare moja dhidi ya Medeama walipocheza hapa nyumbani, ndiyo inaburuza mkia wa kundi hilo ikiwa na pointi moja lakini Pluijm amesema yuko tayari hata kama wamekuja kimyakimya.
Pluijm amesema anafahamu mashabiki wa timu hiyo wana hamu ya kuona wanapata ushindi wa kwanza, hivyo wanafanya kila juhudi kutimiza hilo ambapo anaamini hilo litatimia watakapocheza Jumamosi hii.
“Bado hatujashinda hata mechi moja katika hatua hii, kwa sasa tunafanya kila liwezekanalo ili kushinda mechi ya kwanza dhidi ya MO Bejaia, lakini kwa bahati mbaya kwenye mchezo huo tutamkosa Ngoma ambaye anatumikia adhabu ya kuwa na kadi mbili za njano.
“Hiyo haiwezi kutufanya kushindwa kupambana na kupata ushindi kwani kuna wachezaji walikuwa wana majeraha na wengine walikuwa wanaumwa malaria, wote wamepona na wameanza mazoezi, sasa tupo kamili kwa mechi hiyo,” alisema Pluijm.
0 COMMENTS:
Post a Comment