August 10, 2016

MAVUGO

Baada ya straika mpya wa Simba, Mrundi, Laudit Mavugo kuwapagawisha mashabiki wa timu hiyo kwa uwezo wake mkubwa aliouonyesha juzi, sasa amegeukia kwa Mrundi mwenzake, mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe akianza kwa kutamba: “Hapana, Tambwe haniwezi niko vizuri zaidi yake.”

Mavugo ambaye alikuwa akisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa klabu hiyo, kwa mara ya kwanza juzi aliichezea timu hiyo dhidi ya AFC Leopards ya Kenya katika mchezo maalum wa Simba Day na Simba kufanikiwa kushinda kwa mabao 4-0.

Katika mabao hayo, Mavugo aliyeingia kipindi cha pili, alitoa pasi ya bao la tatu lililofungwa na Shiza Kichuya kabla ya yeye mwenyewe kufunga hesabu kwa kukandamiza bao la nne.

Baada ya mchezo huo, Mavugo aliyetua Simba akitokea Vital’O alianza kwa kuwatuliza mashabiki wa Simba kwa kusema kuwa huo ni mwanzo tu na kwamba bado ana safari ndefu ya kuendelea kufanya vizuri zaidi na kuipa makombe timu hiyo.

“Nimefurahi sana leo (juzi) kuona sapoti kubwa ya mashabiki na wachezaji wenzangu na kufanikiwa kuibuka na ushindi, niseme kuwa huu ni mwanzo tu na kwamba tutaendelea kufanya vizuri zaidi kwa kuwa nia yetu ni ubingwa wa msimu ujao.

“Kuhusu Tambwe, ninamfahamu, najua kwamba ni mfungaji bora wa sasa lakini niseme tutapambana na nitamfunika. Ukiangalia katika ufungaji bora msimu uliopita yeye ana mabao 21 lakini mimi nilifunga 30 kule Burundi.

“Ukirudi katika msimu wa nyuma tena, yeye alifunga 14, mimi nikafunga mabao 32. Sasa unaweza kuona hapo kwa haraka tofauti iliyopo, lakini kingine naifahamu ligi ya Tanzania na ninaifuatilia, kwa hiyo najua ninaokwenda kukutana nao,” alisema Mavugo.

Imeelezwa kuwa vita ya Mavugo na Tambwe inatarajia kuwa kubwa zaidi utakapoanza msimu mpya si kwa kuwa wanacheza katika timu mbili hasimu zaidi Tanzania bali hata katika kuwania namba kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Burundi.

Katika kikosi cha Burundi, kwa sasa Tambwe na straika aliyewahi kuichezea Yanga na Azam, Didier Kavumbagu ndiyo mastraika tegemeo huku Mavugo akiwa kama mbadala wa washambuliaji hao.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV