August 5, 2016


Na Saleh Ally
KIMEPITA kipindi kirefu kidogo kusikia uongozi wa Yanga ukilumbana kupitia vyombo vya habari kwa sababu ya upande mmoja kusema haujatendewa haki.

Nidhamu ya kufanya mambo yaende kwa utaratibu ulio sahihi, iliwasaidia Yanga kubadilisha mambo mengi na kufikia kuanza kuonekana ni klabu ambayo ni mfano wa kuigwa.

Kawaida, kama kuna jambo la kiuongozi, uongozi wa Yanga ulifanikiwa kumaliza kila kitu na huenda kama likisikika, basi si rahisi kusikia kiongozi akilalama kwenye magazeti au redio.

Kwa misimu minne mfululizo, chini ya uenyekiti wa Yusuf Manji, Yanga imechukua ubingwa mara tatu, imeshiriki michuano ya kimataifa misimu yote na safari hii, msimu uliopita imefanikiwa kucheza hadi hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho.

Klabu nyingine nyingi zilikuwa zikitamani mwenendo au mafanikio ya Yanga ambayo mwenyekiti wake kwa kushirikiana na makamu, waliendesha kwa ushirikiano wa karibu na sekretarieti ambayo iliundwa na Wanayanga ambao ninaamini mawazo yao yalikuwa mchango mkubwa katika njia ya maendeleo.

Lakini jana nilimsikia mmoja wa wajumbe wa kamati ya utendaji Salum Mkemi akilalama anaonewa, akilalama hawajui kuhusu mkutano, akilalama kuhusiana na mkataba wa Quality Group na klabu yao.

Kimsingi kwa mtu anayejielewa, atajiuliza maswali mengi na jibu linaweza kuwa moja. Hivi; vipi Mkemi akahoji kuhusiana na yote hayo, kwani mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga hawezi kuzungumza na mwenyekiti wake? Kama amemkosa hawezi kuzungumza na Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga?

Nilimsikia Sanga naye akijibu hoja redioni! Hii kwangu ninaona ni dalili ya Yanga kuporomoka na kama Yanga wenyewe wasipokuwa makini, basi utakuwa ni mwanzo wa anguko lao na mwisho watarejea walipopita kwa miaka mingi sana, naweza kufananisha na kile kipindi cha malumbano ya Mzee Mzimba na mwenyekiti wakati huo, Abbas Tarimba.

Maneno ya Mkemi, huenda yanaweza kujaziwa maswali pia. Kwamba mkutano hauujui, umemuuliza kiongozi wako akakataa? Umehoji kama wamevunja katiba wakakujibuje? Na kwa nini unakuwa na hofu ya kwenda kwenye mkutano.

Mkataba wa Quality umeanza lini? Lakini Yanga inasafiri kwa ndege kila sehemu hadi kupewa jina la Wakimataifa kwa fedha za nani? Sh milioni 36 za TBL kwa mwezi, wakati Yanga inalipa mshahara zaidi ya Sh milioni 100 kwa mwezi. 

Je, unajua zinazojaziwa zinatokea wapi, uliwahi kuhoji haya? Kama hapana kwa nini umeuliza hayo?
Unaweza kugeuka kuwa mjadala wa maswali ambayo majibu yakageuka kuwa magumu kwa Mkemi na wenzake, lakini hii bado haiwezi kuwa sifa ya upande mmoja na kuirudisha Yanga nyuma kwa matakwa ya wengine.

Kama unakumbuka, wakati wa kampeni, kila kiongozi aliyegombea, walioshinda na kushindwa wote walisema wanataka kuusaidia uongozi wa Manji na Sanga kuendeleza mambo mazuri waliyofikia. Ndani ya miezi miwili, wanayaona maendeleo hayo ni duni au tatizo?

Karibu kila aliyepiga kampeni, alizungumzia mafanikio ya uongozi. Kama umeona tatizo, vipi unashindwa kuuhoji uongozi na badala yake ukimbilie kutengeneza kama kuna tatizo?

Sidhani kama uongozi nao utataka kulumbana na upande wa viongozi hao walioingia hivi karibuni. Huenda hawakuwahi kuongoza Yanga kabla au kama waliongoza hawakuwahi kupitia mfumo ambao Yanga wameupitia na kuwapa mafanikio.

Haitakuwa sawa uongozi kurudisha malumbano, badala yake utoe msaada kwa kuwashauri viongozi hao wapya na ikiwezekana kuwaonyesha njia sahihi walizopita hadi kufikia hapo na huenda ikawavutia wengi kuingia kugombea.

Lakini kama kuna sehemu na uongozi utaona umekosea, basi unaweza kusikiliza na kuyafanyia kazi maoni ya kina Mkemi kwa lengo la kujenga kupitia umoja na si malumbano.
Yanga kuweni makini, historia inaonyesha klabu hizi ziliangushwa na kumeguka kutokana na uongozi na si mashabiki.3 COMMENTS:

  1. Kuna baadhi ya watu wameingia kwenye uongozi wakiwa na maslahi binafsi na akili za kishabiki ambazo kwa muda mrefu wanayanga walikwishasahau chini ya uongozi wa Manji.Hawa watu wanapaswa kudhibitiwa mapema wengine waligombea kwenye vyama vya soka DRFA na TFF hivyo wamekwenda Yanga kimaslahi zaidi.Huyu Mkeni juzi juzi tu alikuwa anaongea kwenye kipindi cha Tamasha la Michezo ITV akawa analaumu kwa nini Saidi Makapu hapangwi nafasi ya kiungo mkabaji na pia Niyonzima badala ya kupiga pasi kwenda mbele anapeleka pembeni.Hii ni aina ya kiongozi asiyejua mipaka ya kazi yake na ameathirika na ushabiki

    ReplyDelete
  2. Siwezi kuhukumu iala haki ni bora kuliko nguvu ya pesa. Kilichofanya Yanga kuwa kimya si kwamba walikuwa sahihi bali ni nguvu ya pesa ndio ilikuwa ikiwanyamazisha na wala si haki.

    ReplyDelete
  3. Kijana Saleh Jembe una sifa zote za kuitwa mwandishi wa michezo uliyekamilika na ni mfano wa kuigwa kwa waandishi wenzio kwanza unaelimisha jamii pia kwenye makosa huchelewi kuyaoneyesha hadharani kwa kweli hoja zote ulizozitoa juu ya Yanga ni safi hazina mashaka kama ni mfuatiliaji au mwanachama wa klabu yeyote Tanzania sio Yanga tu yeyote ile unapokuwa na nia ya kutaka kuwa kiongozi wa klabu hapana shaka kabla ya kugombea ni lazima utakuwa umefuatilia kwa undani jinsi gani mapato na matumizi ya timu yanavyokuwa ni ukweli usio pingika udhamini wa timu za Tanzania ni mbovu sana tena ni kiwango cha chini kama ulivyosema matumizi ya Yanga ni milioni 100 kwa mwezi na mdhamini anatoa milioni 36 ni lazima ujiulize hili pengo linazibwa vipi na linazibwa na nani? Ni aibu ilioje kiongozi kuuliza suala la kijinga kwa mkataba ulioingiwa na viongozi uliowakuta klabuni kabla ya ww kuingia tena una hoji kwenye vyombo vya habari si dhani kama kweli huyo uliyemwita Mkema anastahili kuwa kiongozi wa taasisi kama hiyo ya Yanga inafaa kwa ushauri wangu kabla ya kujitokeza kwa kuuliza suala kama hilo kwanza akae chini ajiulize mwenyewe jee hilo jambo alilofanya ni sahihi kwa nini asiulize uongozi anauuliza suala la kipuuzi kwenye vyombo vya habari? Si dhani kama huyo jamaa ana sifa za kuwa kiongozi ni vyema mwenyekit na makamo wake wamuangalie kwa jicho jengine anatawaletea mgogoro usio na maana hapo klabuni kwao.

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV