Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, amewataka wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kutokuwa na hofu ya kutetea ubingwa wao msimu huu kwani ameiona Simba na kubaini kuwa haitishi ukilinganisha na kikosi chao jinsi kilivyo hivi sasa.
Niyonzima juzi aliuangalia mchezo wa Simba na JKT Ruvu kwa kutumia televisheni na akacheka sana baada ya kubaini kuwa nyota wa kikosi hicho wanasifiwa mno tofauti na uhalisia wao wawapo uwanjani.
“Nimewaona Simba, ni wa kawaida kabisa. Uwezo wao ni mzuri lakini hawawezi kushindana na timu kama Yanga. Sisi tumecheza mechi nyingi za kimataifa, tuna uzoefu na tupo fiti tofauti na wao,” alisema Niyonzima alipozungumza na Championi Jumatatu juzi Jumamosi.
Aliongeza kuwa wamejipanga vilivyo kwa ajili ya Ligi Kuu Bara na anaamini kuwa hakuna timu itakayowasumbua msimu huu.
Alisema licha ya kushindwa kufanya vizuri katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, mashabiki hao wasife moyo ila wanachotakiwa ni kuendelea kuwaunga mkono muda wote na kusahau yaliyopita.
“Ndiyo kwanza tumeanza ligi, hivyo nawaomba mashabiki Yanga wasiwe na hofu juu ya kutetea ubingwa wetu msimu huu, Simba nimewaona, wana timu nzuri lakini haitishi kama ilivyo yetu.
“Nawaomba waendelee kutuunga mkono muda wote na mambo mazuri yanakuja kwani tutafanya maajabu makubwa msimu huu,” alisema Niyonzima.
0 COMMENTS:
Post a Comment