August 27, 2016Na Saleh Ally, aliyekuwa Barcelona
UNAPOKUWA nje ya Hispania, unaweza usijue mambo mengi sana hasa kuhusiana na mapito ya timu kadhaa na hasa zile kubwa za Hispania.

Unaweza kusikia mtu anazungumziwa sana na watu wa Barcelona, lakini akawa si anayejulikana hata kidogo kwa Tanzania kwa kuwa Lionel Messi, Neymar, Luis Suarez na wengine wa sasa wanaendelea kushika hatamu.

Jose Maria Bakero Escudero ni kati ya nyota waliofanya vizuri sana wakiwa na kikosi cha Barcelona kuanzia mwaka 1988 hadi 1997, sasa kiungo huyo mwenye kasi wakati huo ana umri wa miaka 53 na amekuwa akiendelea na kazi za ukocha.

Bakero aliitumikia Barcelona kwa miaka tisa na kufanikiwa kubeba makombe 18, likiwemo la Ligi ya Mabingwa Ulaya, pia akaitumikia timu ya taifa ya Hispania katika michuano ya Kombe la Ulaya na pia Kombe la Dunia.

Kawaida ni mtu aliye makini na kazi yake, akiwa kiungo mchezeshaji, katika mechi zake 483 za soka la kulipwa alifunga mabao 139.

Lakini alipata umaarufu mkubwa akiwa mtoa pasi kwa washambuliaji wawili hatari zaidi wa Barcelona wakati huo, Romario kutoka Brazil na Histo Stochkov raia wa Bulgaria.


Bakero ndiye alikuwa nahodha wao wakati huo, huku ndani ya kikosi hicho kukiwa na mmoja wa mabeki kinda, Pep Guardiola ambaye sasa ni kocha wa Manchester City.

Moja ya juhudi za SALEHJEMBE ilikuwa ni kumpata gwiji huyo asiyesikika. Ingawa kulikuwa na ugumu, lakini mwisho, Championi halishindwi kitu, ni suala la muda tu.

Pamoja na ugumu wa kumpata, Bakero alikuwa mcheshi na aliyetoa ushirikiano wa kutosha.
Moja ya mambo aliyosisitiza ni kwamba Barcelona itaendelea kutamba milele kwa kuwa tayari imejaa kwenye mioyo ya watu wa rika la kila aina.


Bakero anasema watoto wanaokua sasa, wengi wanataka kuona Barcelona inaendelea. Waliopo ndani ya Barcelona kama akina Messi wanatamani kufanya bora zaidi na kukizidi kizazi kilichopita.

Lakini wenye umri kama wake, hawako tayari kuona Barcelona inadidimia. Na huo ndiyo ulinzi mkubwa wa klabu hiyo.

“Utaona kuna klabu ya wazee ambayo inaendelea ndani ya klabu. Hawa wakongwe wanatambulika, mimi ni mmoja wao na tuna msaada mkubwa ndani ya klabu.


“Vijana wanataka kuiendeleza, watoto wanaokuwa wanatamani kuwa sehemu ya Barcelona. Hii ndiyo raha ya hii klabu, itaishi milele,” anasema Bakero.

Kuhusiana na enzi zao, wakati huo akicheza pamoja na wachezaji wengi ambao pia walikuwa maarufu na akapewa nafasi ya kuwa nahodha, anasema Kocha Johan Cruyff alimuamini na kamwe hakukosea.


“Sisi ndiyo wachezaji wa kwanza wa Barcelona kuanza kuutumia mfumo wa Tiki -Taka. Unajua unaona Guardiola anautumia sana, lakini kila aliyekuwepo kipindi kile, lazima atautumia.

“Ilikuwa ni rahisi kuwa nahodha kwa kuwa nilifurahia. Kilikuwa ni kitu kipya na mimi nikaonekana ninauwezo na nilikuwa ndiye mchezeshaji hasa kwa pasi za mwisho.

“Tiki-Taka ni uchezaji wa pasi fupi za karibu. Mnatembea pamoja na haraka. Romario alikuwa ni hatari sana, kwanza alifiti kwenye mfumo lakini mara nyingi alifunga mabao, hakuna kati yetu aliyejua kama angefanya hivyo.


“Nafikiri kadiri siku zinavyosonga mbele, timu nyingi sana duniani hata asilimia 70 zitakuwa zinatumia mfumo huo. Unarahisisha mambo mengi sana. Cruyff alikuwa akisisitiza mpira si mbio tu kama riadha, lazima uchezwe na sasa unaona Tiki-Taka ndiyo inavutia zaidi duniani,” anasema.


Katika ufundishaji wake, Bakero anasema ataendelea kufundisha Tiki-Taka, kama itakuwa imeshindikana, basi yupo tayari kuondoka kwenye timu. Anachotaka ni kuona timu inayocheza ndiyo maana karibu kila kocha anayetua Barcelona, anajikuta analazimika kuufuata mfumo huo kwa kuwa ni mfumo mama. “Tangu mabadiliko ya Cruyff kwenda kwenye Tiki-Taka. Barcelona haitauacha na unaona, inazidi kuwa bora duniani kila kukicha. Mfumo huu ni ulinzi mwingine wa milele kwa Barelona,” anasisitiza Bakero ambaye mara ya mwisho aliinoa Juan Aurich ya nchini Peru.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV