Na Saleh Ally aliyekuwa Madrid
KILA sehemu wanaweza kuwa na utamaduni wao. Watu wa Madrid wanaamini ni vizuri kufanya kazi kwa juhudi na ukifanikiwa, kusherekea ni utamaduni.
Real Madrid na Atletico Madrid ndiyo klabu kubwa za Jiji la Madrid, pia ni sehemu ya timu tatu kubwa za nchini Hispania.
Katika ziara ya kisoka nchini humo, niliona vizuri kufika katika minara miwili maarufu ya Cibele na Neptune. Vizuri kwa sisi kuita sanamu.
NIKIWA MBELE YA MNARA WA CILEBES NA JENGO LA MANISPAA YA JIJI LA MADRID AMBAKO NI OFISI WA MEYA WA JIJI HILO. |
Sanamu hizo mbili zinazojulikana kama minara ni maarufu sana sasa duniani kote kwa kuwa Real Madrid na Atletico Madrid huitumia kama sehemu ya kushangilia.
Nilichojifunza ni kwamba minara yote imetengenezwa na wataalamu mbalimbali wa uchongaji lakini mmoja aitwaye Ventura Rodriguez, alishiriki kutengeneza kila upande.
Cibeles na Neptuno, iko karibu kabisa. Ni umbali kama wa mita mia hivi. Wakati fulani, meya wa Jiji la Madrid alitaka kuweka uzio kutoka upande mmoja, kwenda mwingine. Lakini haiwezekani kwa kuwa katikati ni barabara kubwa.
Cibeles:
Huu ni mnara ambao waliuchagua Madrid kwenda kushangilia kila wanaposhinda. Muonekano wake ni mtu ambaye amekaa kwenye toroli huku wanaosukuma liende ni Simba.
Uko mbele ya jengo la Jiji la Madrid, kuna kipindi ulipewa jila la Mnara wa Madrid na Real Madrid wanaitumia kwa kuwa wao ndiyo Madrid, jambo linaonyesha kuwaumiza sana Atletico Madrid.
Kihistoria, inaonyesha Cibeles ni sehemu ya miungu ya Kigiriki na iliyokuwa ina heshima kubwa. Jambo ambalo Madrid wanaona kuwa wao ni watu wa kuheshimiwa na ndiyo wenye jiji. Hivyo wakishinda kombe, wanakusanyika hadi mashabiki 40,000. Kwa kuwa ni sehemu kama keep left, lakini wanajaa kwenye barabara zote kubwa nne na kufanya eneo kuwa halipitiki kabisa.
Neptune:
Wakati Cibeles ni mwanadada mrembo, Neptune ni mwanaume. Mmoja wa wapinzani wa Cibeles katika historia ya miungu ya Kigiriki pia.
Hivyo Atletico Madrid nao wamemchagua kama sehemu yao ya kushangilia kwa kuwa ni mwanaume na mpinzani wa Cibeles.
Kama wakishinda kwa maana ya ubingwa, basi kutoka uwanja wa ndege, kombe linafikia hapo.
Hawataki kujali kwamba hawako karibu na jengo la Manispaa anapopatikana Meya wa Jiji la Madrid. Lakini wanaamini wao ni wanaume na wanaona Neptune ni mwanaume wa shoka.
Historia ya minara hiyo ni ndefu maana historia ya miungu ya Kigiriki ni tangu mwaka 1784, ndipo ikajengwa kwenye jiji la Madrid. Lakini kikubwa, timu hizo mbili, zimejitengea himaya na kinachovutia. Kila upande wa mnara mmoja ndipo mwelekeo wa ulipo uwanja wa timu husika. Ni sawa na kusema, wametenga himaya zao katikati ya Jiji la Madrid.
0 COMMENTS:
Post a Comment