August 17, 2016


Staika wa zamani wa Simba na Stand United, Elias Maguri ambaye sasa anaitumikia timu ya Dhofar ya nchini Oman, ameendelea kufanya vizuri akiwa na kikosi hicho.

Juzi Jumatatu, mshambuliaji huyo aliongoza timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Oman kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 23 ya nchi hiyo.

Hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa Maguri kuiongoza timu yake hiyo kuibuka na ushindi ambapo mara ya kwanza alifanya hivyo katika mchezo wa kirafiki dhidi ya AL Etihad ambayo ipo daraja la pili na sasa inatafuta nafasi ya kupanda ligi kuu.

Maguri alisema kuwa anajivunia hali hiyo kwani inamfanya azidi kuongeza bidii anapokuwa uwanjani ili aweze kuwa na nafasi ya kudumu katika kikosi cha timu hiyo itakayomwezesha kuonwa na klabu nyingine za ndani na nje ya nchi hiyo.

“Namshukuru sana Mungu kwani maendeleo yangu tangu nimefika hapa siyo mabaya sana na nimekuwa nikifunga katika mechi zote nilizocheza ambapo leo (juzi Jumatatu), tulikuwa na mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 23, nimeifungia timu yangu bao moja ambalo tulipata katika mchezo huo.


“Lakini pia kama wiki mbili zilizopita, niliifungia pia timu yangu bao moja katika ushindi wa mabao 2-1 tulioupata, hivyo najivunia hali hiyo na ninamuomba Mungu anijalie niendelee hivihivi,” alisema mshambuliaji huyo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV