August 10, 2016


Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, juzi alipishana na bao kali lililofungwa na mshambuliaji wa Simba, Mrundi, Laudit Mavugo.

Mholanzi huyo, alipishana na bao hilo wakati Simba ilipocheza na AFC Leopards inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya katika sherehe ya Simba Day ambayo timu hiyo ilitimiza miaka 80 tangu kuanzishwa kwake.

Katika mechi hiyo, Simba ilisherehekea siku hiyo kwa furaha kubwa ya ushindi wa mabao 4-0 ambayo yalifungwa na Ibrahim Ajib aliyefunga mawili, Mavugo na Kichuya kila mmoja akifunga moja.

Pluijm alifika kwenye sherehe hizo zilizofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam mapema kabla ya mechi kuanza akiwa ameongozana na msaidizi wake Juma Mwambusi.

Kocha huyo alifika uwanjani hapo kwa ajili ya kuzisoma mbinu za Mcameroon, Joseph Omog na kuwajua wachezaji hatari ili watakapokutana kwenye Ligi Kuu Bara ajue jinsi ya kuwadhibiti wachezaji hatari.

Wakati mechi hiyo ikiendelea, kocha huyo alionekana kuandika baadhi ya vitu kwenye karatasi yake aliyokuwa nayo mkononi akiwa amekaa kwenye jukwaa kuu na Mwambusi huku wakijadiliana baadhi ya vitu kila mara.

Wakati akiyashuhudia mabao ya Ajib na Kichuya, kocha huyo hakuliona bao la Mavugo alilolifunga dakika ya 82, akimalizia shuti la Kichuya alilolipiga kabla ya kipa wa Leopards, Ian Otieno kuutema ndani ya sita.


Katika mechi hiyo, Pluijm aliondoka dakika ya 75 kabla ya kumalizika ambapo aliongozana na Mwambusi waliofika wote uwanjani hapo na nyuma yake ndipo Mavugo akafunga.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic