Unaikumbuka ile ishu ya kiungo mkabaji wa zamani wa Yanga, Athumani Idd ‘Chuji’ alivyoanza kuichezea timu hiyo? Basi ndiyo beki wa pembeni, Hassani Kessy atakavyocheza Jangwani msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Ishu ilikuwa hivi, Chuji aliondoka Simba na kwenda kusaini Yanga baada ya mkataba wake kumalizika, lakini baadaye Simba wakaibuka na kudai mchezaji huyo bado ana mkataba wa kuichezea timu hiyo kitu ambacho hakikuwa sahihi.
Sakata hilo, linafanana na la Kessy ambaye alisaini mkataba wa miaka miwili ya kuichezea Simba hivi karibuni mara baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu uliopita, lakini baadaye Simba wakaibuka na kudai kuwa beki huyo alisaini Yanga akiwa bado ana mkataba Msimbazi.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, alimtoa hofu beki huyo kwa kumwambia wala asiwe na hofu, suala lake litamalizika na ataichezea timu hiyo msimu ujao wa Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika, mwakani.
Manji alisema hiyo siyo mara ya kwanza Yanga kukumbana na tatizo kama hilo, ilitokea kwa Chuji viongozi wakapambana na baadaye akaachiwa kucheza baada ya kugundulika mkataba wake ulimalizika.
Aliongeza kuwa, kwa kipindi chote hicho ambacho Kessy yupo nje ya uwanja, wataendelea kushirikiana naye kwa kila jambo ikiwemo kupewa mshahara wa kila mwezi na posho kama walivyokuwa wachezaji wengine.
“Kessy hatakiwi kuwa na hofu kabisa, kila kitu kinaenda kwa kufuata utaratibu, uongozi unatambua kuwa watani wetu Simba hawataki kumpa barua ya kumuidhinisha kuichezea Yanga, hivyo sisi hatuwezi kulazimisha, sisi tunasubiri kanuni na sheria zitumike kuamua jambo hilo.
“Hiyo siyo kesi ya kwanza Yanga kuipata, tukio kama hilo liliwahi kumtokea Chuji wakati anasaini kuichezea Yanga, baadaye suala likawa kubwa baada ya Simba kudai kuwa Chuji alikuwa ana mkataba na timu hiyo, lakini baada ya TFF kukutana na kulijadili suala hilo, ikiwemo kupitia mikataba yote, iligundulika kuwa Chuji alimaliza mkataba.
“Ninaamini kuwa, staili iliyotumika Chuji kuruhusiwa kuanza kuichezea Yanga rasmi, basi ndivyo itakayotumika kwa Kessy,” alisema Manji.
0 COMMENTS:
Post a Comment