September 17, 2016

Mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajib, juzi jioni alishindwa kumaliza mazoezi ya timu yake baada ya kuumizwa kifundo cha mguu na beki Novaty Lufunga, lakini jana aliweza kujifua mwanzo mwisho.

Katika mazoezi hayo ya juzi kwenye Uwanja wa Boko Veterani jijini Dar es Salaam, Ajib alitolewa uwanjani akiwa amebebwa baada ya Lufunga kumuumiza mguu wa kushoto na kuzua hofu.


Baadhi ya mashabiki wa Simba waliokuwepo mazoezini hapo, walionyesha hofu ya kumkosa Ajibu katika mchezo wa leo dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.


Hata hivyo, jana Ijumaa asubuhi Ajibu alifanya mazoezi na wenzake kwenye Uwanja wa Jeshi wa Ndege Beach uliopo nje kidogo ya Dar es Salaam. 


Akizungumzia hali yake, Ajib alisema: “Ningefurahi kama ningecheza dhidi ya Azam lakini ndiyo hivyo sina uhakika, hapa natazama hali yangu itakavyokuwa Jumamosi (leo).”


Daktari wa Simba, Yassin Gembe kwa upande wake alisema: “Ajibu anaendelea vizuri, ila uhakika wa kucheza dhidi ya Azam tutaupata kesho (leo), tunamshukuru Mungu kwa hatua hii aliyoamka nayo leo (jana).”


Kwa mujibu wa Gembe, kiungo Mwinyi Kazimoto ana wasiwasi wa kukosa mechi ya leo kwani anasumbuliwa na maumivu ya nyonga.


SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV