September 14, 2016

Beki anayefanya vema kwenye kikosi cha Yanga na ambaye amekuwa akipata nafasi ya kuzanza kwenye kikosi cha kwanza, Andrew Vincent ‘Dante’, amemtolea uvivu kiungo anayesumbua Shiza Kichuya wa Simba kwa kusema kuwa anamjua nje-ndani, hivyo si mtu wa kumsumbua iwapo atapangwa kwenye mchezo wa Oktoba Mosi, mwaka huu wakati miamba ya soka la Bongo, Simba na Yanga zitakapomenyana.

Dante amegeuka lulu ghafla Jangwani kutokana na kiwango cha juu anachokionyesha kwenye safu ya ulinzi katika mechi tano alizoichezea timu hiyo tangu ajiunge nayo akitokea Mtibwa Sugar.

Mavugo


Kichuya

Akizungumza na Championi Jumatano, kuelekea mchezo wa Oktoba Mosi, Dante alisema hana hofu yoyote na ‘kiberenge’ Kichuya ambaye amekuwa tishio kutokana na kasi, chenga na pasi zake kwenye kikosi cha Simba.

 Beki huyo ambaye ni shabiki wa kutupwa wa beki Mbrazili, Dante Bonfim Costa anayekipiga Nice ya Ufaransa alipo mtukutu, Mario Balotelli alisema Kichuya wa Mtibwa ni yuleyule na mbinu zake za kumdhibiti anazijua fika, ila anamhofia sana Mavugo.

Anaomba iwapo atapangwa siku hiyo, apewe kazi ya kumchunga winga huyo waone kama ataweza kufurukuta.

Dante

“Kichuya ni yuleyule. Kichuya wa Mtibwa na wa sasa (Simba) kiukweli sijaona tofauti yake. Hajabadilika. Mbinu zake za kuwatoka mabeki ni zilezile na mimi ninaujua vema ujanja wake na muda gani unatakiwa kumfanyia ‘timing’ ya kumdhibiti ili asilete madhara. Bahati nzuri nimekuwa naye Mtibwa nina kila kitu chake.

“Sijui, lakini kama nikifanikiwa kucheza mechi hiyo, watanisumbua wengine kina Mavugo lakini siyo Kichuya. Hii haimaanishi ni mchezaji mbaya, mimi nazungumzia mbinu zake anazozitumia kusumbua timu pinzani,” alisema Dante.

Katika mechi tano hizo alizochezea Yanga, Dante amefanikiwa kucheza sanjari na mabeki wakongwe Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Vincent Bossou na Kelvin Yondani kwenye michezo tofauti.

SOURCE: CHAMPIONI



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic