September 17, 2016

Na Saleh Ally, Barcelona
Wapenda michezo wanaijua Klabu ya Barcelona kama ni ya soka pekee, lakini ukweli ina aina mbalimbali za michezo kama kikapu, hockey na mingineyo inayofanya vizuri.


Umaarufu wa Barcelona, uko kibiashara zaidi. Pamoja na timu yake kuwa gumzo kutokana na kufanya vizuri, lakini utendaji wake kibiashara unapanda kwa kasi kubwa sana, kila kukicha.Mkataba wa Barcelona na kampuni maarufu ya kutengeneza saa ya Maurice Lacroix, awali ulionekana kuwashangaza wengi sana.Baadhi wakiwemo wataalamu wa masuala ya uchumi na biashara waliona haikuwa sawa. Bidhaa za kampuni hiyo maarufu ya utengenezaji saa kutangazwa na klabu hiyo walidhani ingekuwa bora zingetangazwa na waogeleaji au wakimbiaji.


Lakini wamiliki wa Maurice Lacroix walisisitiza Barcelona inaweza kuwa msaada mkubwa kwenye biashara yao kutokana na kukua kwa kasi sana.Kweli, biashara ya saa za Barcelona zilikuwa zikivaliwa na wachezaji na kutangazwa. Pia wao ndiyo wamekuwa wakizivaa kila wanapokuwa kwenye sehemu zenye watu wengi kama sehemu ya matangazo.


Mafanikio yamekuwa makubwa na kuwashangaza wengi sana, kwani Maurice Lacroix wameeleza ndani ya siku 18, wateja na watu wanaozijua saa za Maurice Lacroix walipatikana 400,000 ambao ni wapya.
Kukua huko kwa haraka kuliwatisha. Kwa kuwa saa zao zilitangazwa na wachezaji wachache tu akiwemo Gerard Pique ambaye tangu awe katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamuziki Shakira, amekuwa kipenzi cha akina dada.


Inaelezwa, wanawake ndiyo walionunua kwa wingi sana saa za Maurice Lacroix na Pique alichangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji au mvuto kuzinunua bidha hizo.


Nilijaribu kufuatilia zaidi na kutaka kujua kuhusiana na saa za Maurice Lacroix ambazo zinakuwa na nembo ya Barcelona.


Katika moja ya maduka ya Uwanja wa Kimataifa wa Barcelona, saa moja ya Maurice Lacroix inauzwa hadj euro 3505 (zaidi ya Sh million 7.5).


Si kwamba hakuna saa za bei ya chini, lakini nyingi angalau hadi Sh 500,000 za Tanzania au zaidi ya hapo. Jambo ambalo limeikuza biashara za moja ya kampuni hiyo kongwe ya saa duniani.


Kukua kwa haraka kwa solo la saa hizo za Barcelona, Maurice Lacroix wameona wanapaswa kuendelea kujitanua zaidi katika klabu. Sasa wameingia mkataba na klabu ya nyumbani kwao ya FC Basel.


Kama hiyo haitoshi, wametangaza kuingia mkataba na klabu nne za Bundesliga lakini lengo ni kutanua wigo wao na kuwaonyesha waliokuwa wanafikiria wamekosea, wao ndiyo walikosea.


Unaona sasa, Barcelona inaonekana kuwa ni bango sahihi la matangazo. Kwani hadi vinavyoonekana ni vigumu kufanikiwa kwa klabu hiyo, inakuwa ni rahisi sana.

 

Hii inatokana na mpangilio mzuri na namna ambavyo imejipanga kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi juu na huenda kwa mwendo huo, watafanikiwa zaidi kuliko klabu nyingine. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV