Na Saleh Ally
WIKI iliyopita, kauli mbili zilikuwa gumzo zaidi katika nyanja ya michezo na zote zilitolewa na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohammed Kiganja.
Kwanza alianza kuhusiana na mchezo wa ngumi za kulipwa na kusisitiza kwamba mashirikisho yote yawe yanachukua kibali kwenye shirikisho moja ambalo ni TPBC.
Tayari viongozi wa mashirikisho mengine kama PST, TPBO na mengine yameeleza nia yao ya kupinga kwa nguvu na dhati jambo hilo ambalo wameliita la ajabu huku wakisisitiza kutaka barua kutoka kwa Kiganja badala ya vile walivyosikia kauli yake kwenye vyombo vya habari.
Wamesema wamekuwa wakimpigia Kiganja hapokei. Kwangu naona kama Kiganja na serikali wanaweza kuwa na nia nzuri lakini wamelifanyia kazi suala hilo kwa haraka bila ya kulichunguza.
Mimi pia sijawahi kusikia WBC wanachukua kibali kwa WBA kuandaa pambano. Hayo yote ni mashirikisho ya ngumi za kulipwa. Ile si ridhaa na vizuri wakawa huru ingawa udhibiti wa serikali ni jambo jema maana kwenye mashirikisho ya michezo, wanataka kufanya michezo ni sehemu kama shamba la bibi na watu hawadhibitiwi hata kidogo. Wawe huru tu hata kama wanafanya madudu, hili si jambo jema.
Kauli ya pili ya Kiganja ilikuwa ni kuhusiana na suala la Rais wa TFF, Jamal Malinzi achague moja; kwamba abaki na nafasi hiyo au ile ya Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Kagera.
Kwenye hili, huenda Malinzi akajitetea sana kwamba katiba haimzuii. Wale ambao wanaamini anafanya jambo jema nao wanaweza pia wakamtetea kweli, huenda hata kutoa mifano ya kijinga kabisa isiyoendana.
Nimesikia wengine wanatoa ule mfano kwamba rais aliyepita wa TFF, Leodegar Tenga alikuwa katika shirikisho hilo pia Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa)!
Wakati mwingine unajiuliza hawa watu wanafikiria vipi, unajiuliza hawaoni aibu kuchangia wakionekana wanatoka kwenye mstari. Lakini unaweza kusema, wanachofanya ni kuangalia zaidi wanafanikiwa au kupata nini na si taifa linapata nini.
Katiba inaweza kuwa inamlinda Malinzi katika hili lakini ukweli, huu ndiyo wakati wa kuachana nayo na kuhakikisha linabadilishwa. Kiganja alichosema ndicho Malinzi anapaswa kukifanyia kazi.
Hivi, Malinzi analazimisha nini kutaka awe mwenyekiti Kagera, wakati TFF imefeli, haifanyi mambo kwa ufasaha. Ligi imeporomoka, viwango vya waamuzi vimeyumba, Tanzania inazidi kuporomoka. Timu ya taifa ya wanaume na ile ya wanawake hakuna cha maana kinachokifanyika na hakuna hata nafuu.
Sasa kwa nini asitumie muda wa kutosha akiwa kiongozi wa TFF ambalo ni jukumu kubwa. Afanye kazi yake kwa ukaribu zaidi ili kuhakikisha baada ya muda mambo yanabadilika.
Wakati TFF haifanyi vizuri na imerudi nyuma hata ukifananisha na kipindi cha Tenga, ameshindwa kutimiza ahadi rundo wakati anaingia. Vipi tena anajitwika mzigo mwingine ya uenyekiti wa mkoa?
Kagera Sugar imekuwa ikilalamikiwa kwamba inabebwa na waamuzi kwa kuwa wanataka kumfurahisha rais wa TFF. Leo watu wanasema nyasi bandia zimepelekwa Kaitaba, Bukoba wakati ilikuwa sahihi ziwekwe CCM Kirumba kwa kuwa yeye ni mwenyekiti wa Kagera. Hizi zinaweza kuwa hisia tu za wadau, lakini hali halisi inafanya wahisi hivi.
Malinzi aachane na kuangalia kura pekee kwa kuwa ni mwenyekiti wa mkoa, hivyo naye atajipigia kura siku ya uchaguzi. Au isiwe mawazo ya kupata nafasi ya kuingia chumba cha wapiga kura ili kuweza kufanya fitna vizuri siku ya uchaguzi.
Kiganja katika hili; yuko sawa kabisa bila ya kujali utaratibu wake. Malinzi hajafanikiwa hivyo TFF kiasi cha kutaka kujiongezea majukumu tena.
Pia, amekuwa akihoji, kwamba vipi watu hawakuhoji awali. Jibu ni hivi; amegombea mara nyingine tena, watu ndiyo maana wamehoji kwa kuwa alishindwa kujiongeza maana alifeli awali akiwa na hizo kofia mbili, basi ilikuwa vizuri kujipunguzia majukumu ili afanye vizuri upande mmoja.
Sasa ameongeza afeli zaidi? Akumbuke anatufelisha Watanzania, hivyo BMT kuingilia kati ni jambo jema kwa sababu, TFF si ya Malinzi pekee, ni mali yetu Watanzania, mimi na wewe.
0 COMMENTS:
Post a Comment