September 10, 2016

Na Saleh Ally, Barcelona
MECHI ya watani na wapinzani wakubwa katika Jiji la Manchester, kwa mara ya kwanza imeingia kwa kiwango cha juu zaidi katika hisia za kishabiki za wapenda soka nchini Hispania.


Man United watakuwa wenyeji wa Man City kwenye Uwanja wa Old Trafford jijini Manchester leo Jumamosi. Mechi ambayo imegeuka kuwa sawa na El Clasico, mechi maarufu ambayo huwakutanisha watani wakubwa na wapinzani wa hali ya juu, Barcelona na Real Madrid.
 


Upinzani huo unahamia England kutokana na makocha wawili, Jose Mourinho wa Man United na Pep Guardiola aliyeifundisha Barcelona kwa mafanikio makubwa.

Wote wawili wamewahi kufanya kazi nchini hapa wakiwa makocha na wachezaji. Mourinho alikuwa kocha msaidizi wa Barcelona baadaye akawa kocha mkuu wa Madrid lakini Guardiola alikuwa mchezaji tegemeo wa Barcelona na baadaye kocha mwenye mafanikio.
 

Kuwepo kwao kuliamsha ushindani mkubwa kwenye Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ na Guardiola alimkaribisha tena Mourinho kwa kipigo cha mabao 5-0. Lakini baadaye, Mourinho alionyesha mabadiliko na kuanza kushinda dhidi ya mpinzani wake huyo.
 

Watu wa Jiji la Barcelona asilimia kubwa hasa wale wanaoiunga mkono Barcelona wanapenda kuona Mourinho anapokea kipigo kutoka kwa Guardiola ambaye wanaamini ni kijana aliyepata matunzo bora kabisa ya uchezaji soka, pia ukocha.
 

Wengi walio Barcelona wanaiunga mkono Man City kwa kuwa mchezaji na kocha wao wa zamani atakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Mourinho ambaye wakati fulani aliwahi kuonekana ni kama namba moja wa FC Barcelona na Jiji la Barcelona.
 

Kufungwa kwa Guardiola ni sawa na wao wamepoteza. Kawaida nyota wengi wa Barcelona huendelea kubaki kuwa ni watu wa Barcelona na ndivyo ilivyo kwa Guardiola ambaye anaonekana amekwenda kutafuta maisha.
 

Magazeti makubwa ya michezo ya Marca na AS ya nchi hapa, yamekuwa wakiijadili mechi hiyo na hasa msisimko mkubwa kuangukia Hispania kwa mara ya kwanza, maana kabla ingeweza kuchezwa huku watu wakiwa hawajui lolote, lakini wengi watakaa kwenye runinga kuishuhudia.
Mashabiki wengi wa Real Madrid wao wanaona wanaweza kuishangilia Man United kwa kuwa itaongozwa na kocha wao wa zamani, Mourinho lakini usisahau, huko ndipo alipotokea mshambuliaji kipenzi chao, Cristiano Ronaldo.
 

Mtu wa Real Madrid anaona Manchester United ni kama ndugu yao wa England. Na sasa undugu huo unazidi kwa vile watafurahi kuona Guardiola anapoteza.

Guardiola ni kijana wa Barcelona na kufanya vema zaidi ni kama kuendelea kuitangaza Barcelona kwa mlango wa nyuma. Hivyo dua zinaendelea ili kuhakikisha Man City anakiona cha moto.
Hata hivyo, uchunguzi wa Championi unaonyesha kuna kundi la tatu ambalo lenyewe ni lile lenye misimamo bila ya kujali Real Madrid au Barcelona.


Hili kundi ni la Wahispania wengi wapenda soka, wao wanaona Man City ni timu inayofundishwa na Mhispania na inapaswa kushinda na hawaoni sababu ya kumuunga mkono Mourinho kwa kuwa ni raia wa Ureno.


Nimeelezwa ilikuwa aghalabu sana kumuona kijana kavaa nguo ya Man United au Man City katika kipindi hiki. Kawaida huvaa jezi au fulana za timu zao mbalimbali zinazoshiriki La Liga na wengi hawafuatilii kabisa Premier League.


Lakini safari hii inaonekana Mourinho na Guardiola wameweza kuleta ushindani wa juu ambao unawalazimisha mashabiki kuingia upande wa Ligi Kuu England.


Inaonekana kama timu zitaonyesha soka safi katika mechi ya leo, basi kuna uwezekano wa Premier League au Manchester Derby kupata umaarufu wa kasi kubwa na huenda ndiyo itakuwa mpinzani mkubwa kwa ile ya El Clasico ambayo inazikutanisha Barcelona na Real Madrid.
 Fin.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV