September 8, 2016



Makocha Jose Mourinho wa Manchester United na Pep Guardiola wa Manchester City wanatarajia kukutana kwa mara ya kwanza katika Premier League, Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Old Trafford.

Kutokana na viwango ambavyo wachezaji wa timu hizo wamevionyesha tangu kuanza kwa msimu huu, vikosi vyao ambavyo vina thamani ya pauni milioni 620.1 kwa wale wanaotegemewa kuanza kesho, vinatarajiwa kupangwa kama ifuatavyo vikiambatana na thamani zao wakati wakisajiliwa:

MANCHESTER UNITED
David De Gea,
Pauni 17.8m

Alitua mwaka 2011 akitokea Atletico Madrid, enzi hizo bosi wa United alikuwa Sir Alex Ferguson, alianza taratibu lakini sasa ndiye kipa namba moja kikosini hapo.

Antonio Valencia
Pauni 16m

Mwaka 2009 alitua akitokea Wigan Athletic, alitajwa kuwa mbadala wa Cristiano Ronaldo lakini hakutaka presha hiyo kubwa akaamua kubadili namba ya jezi 7 aliyopewa awali ambapo ilikuwa ikivaliwa na Ronaldo na kuvaa namba 25. Alikuwa winga lakini sasa ni beki wa kulia.

Eric Bailly
Pauni 30m

Beki wa kati aliyeanza vizuri licha ya kuwa na muda mfupi tangu aliposajiliwa msimu huu akitokea Villarreal.

Daley Blind
Pauni 13.8m

Alisajiliwa enzi za utawala wa Louis van Gaal mwaka 2014, alikuwa hana nafasi inayoeleweka, ametulia katikati na kuonyesha kuelewana na Bailly.

Luke Shaw
Pauni 30m

Alitua mwaka 2014 kuziba nafasi ya Patrice Evra aliyetimkia Juventus, lakini aliumia na kuwa nje muda mrefu. Beki huyo wa zamani wa Southampton amerejea na kuonyesha yuko fiti.

Paul Pogba
Pauni 89m

Kijana aliyerejea ‘nyumbani’ akitokea Juventus wiki kadhaa zilizopita. Ameweka rekodi ya kusajiliwa kwa dau kubwa, bila shaka ana kazi nzito ya kuuthibitishia ulimwengu kuwa anaweza kufanya kazi.

Marouane Fellaini
Pauni 27.5m

Alipotua mwaka 2013 kulikuwa na mategemeo mengi kutoka kwake, akashindwa kuyafikia, akawa anapanda na kushuka, anaonekana kuzoea kile ambacho Mourinho anakihitaji kutoka kwake.

Juan Mata
Pauni 37.5m

Alisajiliwa na David Moyes mwaka 2014 akitokea Chelsea baada ya kuvurugana na Mourinho ambaye alikuwa Chelsea, wawili hao wamekutana tena lakini safari hii wanaonekana kuelewana.

Wayne Rooney
Pauni 25.6m

Mkongwe wa timu ambaye alitua mwaka 2004 akiwa bado chipukizi, ndiye nahodha na ana uzoefu mkubwa wa mechi hizo za derby.

Anthony Martial
Pauni 57.6m

Alitua mwaka jana akiwa siyo maarufu, kasi aliyoanza nayo imesababisha dunia ya soka impe heshima, msimu huu kasi yake imekuwa ya kusuasua.

Zlatan Ibrahimovic
Huru

Alisajiliwa hivi karibuni akiwa mchezaji huru baada ya kumalizana na PSG. Licha ya umri wake wa miaka 34, lakini ameendelea kuonyesha kuwa anaweza kupambana na kufunga mabao.
JUMLA: PAUNI MILIONI 344.8   



 MANCHESTER CITY

Claudio Bravo
Pauni 17m

Guardiola amemsajili akitokea Barcelona baada ya kutoridhishwa na uwezo wa Joe Hart, bado hajaonekana uwanjani akiwa amevaa jezi ya City ila ni mzoefu anaweza kuanza golini kesho.

Bacary Sagna
Huru

Alisajiliwa akiwa mchezaji huru akitokea Arsenal mwaka 2014. Kocha wake ameonyesha kumuamini yeye zaidi ya Pablo Zabaleta ambaye ni mshindani wake wa namba katika nafasi ya ulinzi wa kulia.

John Stones
Pauni 47m

Everton ilimruhusu beki huyo kutua City wiki kadhaa zilizopita baada ya dau kubwa kuwekwa mezani. Beki huyo wa kati anatarajiwa kukutana na Zlatan kama mpinzani wake mkuu.

Nicolas Otamendi
Pauni 28.5m

Aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Manuel Pellegrini alimsajili mwaka jana ili kuongeza nguvu katika safu ya ulinzi wa kati baada ya kulegalega.

Gael Clichy
Pauni 7m

Naye alitokea Arsenal mwaka 2011 ili kuongeza nguvu katika safu ya ulinzi wa pembeni.

Fernandinho
Pauni 34m

Alitokea Shakhtar Donetsk mwaka 2013, sifa yake kubwa ni kukaba kwa nguvu katika kiungo cha ukabaji ili kuwapa nguvu wale wanaoshambulia kuwa huru kufanya yao.


Raheem Sterling
Pauni 49m

Winga aliyetokea Liverpool, mwaka jana, ameonekana kuwa na mwanzo mzuri tangu Guardiola alipoanza kazi mapema msimu huu.

David Silva
Pauni 24m

Alisajiliwa akitokea Valencia mwaka 2010, tangu hapo amekuwa chachu nzuri katika safu ya kiungo akiwa na uwezo mkubwa wa kutengeneza mashambulizi na kufunga.

Kevin De Bruyne
Pauni 55m

Alikuwa Chelsea, akaonekana hafai, akauzwa kwenda Wolfsburg, lakini miezi 18, yaani mwaka 2015 alirejea England na kujiunga na City, amekuwa mchezaji muhimu kikosini hapo.

Nolito
Pauni 13.8m

Ametua mwaka huu na amekuwa na mwanzo mzuri, hana umaarufu mkubwa lakini kazi yake katika kutengeneza mashambulizi imekuwa nzuri hasa anapotokea pembeni.

Kelechi Iheanacho
Huru

Anaweza kupata nafasi kwa kuwa straika aliyenunuliwa kwa kapuni milioni 38, Sergio Aguero hatakuwepo. Ametokea katika timu ya vijana na sasa ni kazi kwake kuthibitisha ubora wake.

MAN CITY JUMLA: PAUNI 275.3M




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic