September 23, 2016



Na Saleh Ally
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), haliwezi kuwa na kitu kikubwa sana cha kujivunia mafanikio waliyoyapata Kilimanjaro Queens kubeba Kombe la Chalenji.

Dada zetu wamebeba ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati ikiwa ndiyo mara ya kwanza michuano kwa wanawake inafanyika katika ukanda huu.

Hongera kubwa kwao, walichokifanya ni ujumbe kwa TFF na wadau wengine kwamba akina dada wanataka kuinuka, hivyo washikiliwe ili siku moja waonyeshe taifa hili linaweza hata kufikia Kombe la Dunia.

Ukikiangalia kikosi hicho, sasa Asha Rashid ‘Mwalala’, ndiye nahodha, akionekana kuwa mmoja wa wachezaji wakongwe zaidi, lakini mimi nakumbuka mbali zaidi kuhusiana na Twiga Stars ambayo asilimia 90 ya wachezaji wake ndiyo walioibebesha Kilimanjaro Queens ubingwa huo.

Lakini Mwalala, alikuwa mmoja wa wachezaji chipukizi wa Twiga Stars, miaka minne mitano iliyopita. Sasa ni nahodha na mchezaji mkongwe, hii inaonyesha huko nyuma kulikuwa na safari ndefu hadi leo wamefikia hapo.

Safari hiyo ilikuwa ndefu na ilianza kabla ya Jamal Malinzi hajaanza kuongoza TFF, Mwesigwa Selestine hajawa katibu mkuu wa Yanga na baadaye TFF, hii ndiyo maana yangu.

Kwamba wakati sherehe zinaendelea basi ni vizuri sana, mchango wa waliopambana na soka la wanawake hapa nchini, nao ukumbukwe na wapewe thamani yao, si kuendelea kusema pongezi TFF, pongezi nanihii.

TFF tunapaswa kuipongeza kwa kuwa katika kipindi hiki husika, kweli imehusika na mafanikio haya kwa kuihudumia timu hiyo hadi kufikia kutwaa ubingwa. Hongera sana.

Lakini, hawakuianzisha timu hiyo, hawakuikuza timu hiyo, waliipokea kutoka kwa TFF iliyokuwa chini ya Leodegar Tenga na makatibu wake kadhaa kama Frederick Mwakalebela na Angetile Osiah. Kuendelea kuipongeza TFF peke yake, nayo ikasahau kuwahusisha walioupigania mpira wa wanawake, haitakuwa sawa.

Waanzilishi wa timu ya Sayari FC, hawa ni watu wanaopaswa kutafutwa na kushirikishwa kwenye hafla zinazoihusu timu hiyo baada ya kuwa imewasili nchini hiyo jana.

Wadau kama Dk Tamba, huyu alikuwa mlezi wa Mburahati Queens, iliyokuwa na upinzani mkubwa na Sayari. Alikodi nyumba, aliwahudumia wachezaji kwa fedha zake za mfukoni na mwisho walipata mafanikio. Chimbuko lake, ndiyo mafanikio haya ya sasa.

Dk Damas Ndumbaro ambaye ni mmoja wa walimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kile Huria, yaani OUT, huyu pia alipambana kwa ajili ya timu za wanawake, akitoa fedha zake za mfukoni na ndoto yake ilikuwa kuona siku moja wanapata mafanikio makubwa. Leo yamepatikana, basi ashirikishwe.

Mimi ninaamini, hakuna kiongozi wa TFF anayeweza kujisifia kwamba ametoa fedha zake za mfukoni kwa ajili ya soka la wanawake, kama ambavyo waanzilishi wa Sayari, Dk Tamba, Dk Ndumbaro, Dada Furaha na wengine wengi walivyojitoa huko nyuma kutengeneza msingi bora.

Vizuri kabisa kama litakuwa ni jambo jema kama nao watashirikishwa kuonyesha thamani ya kile walichokifanya wakati wakipigania mafanikio. Hili litakuwa ni jambo bora kabisa. Lakini pia niwakumbushe TFF, kwamba sasa wana deni, tena kubwa.

Msingi uliojengwa na wengine, leo ndiyo jambo la kujivunia kwa Watanzania na kupatikana kwa mafanikio katika soka la wanawake. Sasa TFF wana deni kwa kuwa wanapaswa kuyaendeleza hayo.

Isije ikawa wamemaliza huku wakiweka kumbukumbu kwamba wanacho cha kujivunia maana timu iliwahi kutwaa ubingwa wa Cecafa.

Kinachotakiwa, TFF nao ni kuonyesha kwamba waliyaendeleza mafanikio hayo, sasa ni kuisimamia vizuri timu hiyo ivuke hapo na kufika mbali zaidi.


Siku wakiondoka, basi waikabidhi kwa wengine, nao watawakumbuka kutokana na walichokifanya na kukiwa na mafanikio zaidi, tutawakumbusha pia kwamba wasiisahau TFF ya Malinzi, hata kama ilikuwa ina madudu rundo, kuna sehemu ilijitahidi na ijumuishwe kwenye kusherehekea.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic