September 12, 2016

Baada ya juzi Jumamosi, mshambuliaji wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe kuiongoza timu yake hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Majimaji FC, amewataka wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kutulia na kupuuzia kejeli zote wanazopewa na wenzao wa Simba.

Baada ya hivi karibuni kikosi cha Yanga kutupwa nje ya michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika, mashabiki wa timu hiyo walikuwa na wakati mgumu kutoka kwa wenzao wa Simba kuwakejeli kwa maneno mbalimbali ya karaha.


Kutokana na hali hiyo Tambwe, ameliambia Championi Jumatatu kuwa ili aweze kuwaziba midomo lazima awafunge Simba kwa mara nyingine tena watakapokutana uwanjani Oktoba Mosi, mwaka huu.


Alisema licha ya mashabiki wa Simba kujivunia kikosi chao hicho kuwa msimu huu kipo vizuri, yeye anakiona kuwa ni cha kawaida kama  kilivyo cha Majimaji.


Tambwe, siku alipowafunga Simba mapema mwaka huu.
 “Mabao haya mawili niliyofunga leo naweza kusema kuwa nilikuwa napasha misuli moto kwa ajili ya mechi yetu na Simba, kwani nimepania kuhakikisha siku hiyo ninawanyoosha tena kama nilivyofanya msimu uliopita katika mechi zote mbili.

“Mashabiki wao wamekuwa wakichonga sana tangu kuanza kwa msimu huu, hivyo nataka niwazibe midomo yao siku hiyo nitakapowafunga kwa mara ya tatu, nawaomba mashabiki wa Yanga kuwa watulivu na wajiandae kushangalia kwa sana siku hiyo,” alisema Tambwe ambaye juzi Jumamosi iliifungia Yanga mabao mawili kati ya matatu ambayo timu hiyo ilishinda dhidi ya Majimaji FC kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.


Msimu uliopita, Tambwe aliifunga Simba bao moja katika mchezo wa raundi ya kwanza ya ligi Septemba 26, 2015 na kuiongoza Yanga kushinda 2-0. Bao lingine lilifungwa na Malimi Busungu. Katika mchezo wa pili, Tambwe alifunga tena bao moja Yanga ilipopata ushindi kama huo wa raundi ya kwanza. Bao lingine lilifungwa na Donald Ngoma.

 

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV