Ivory Coast imeiondoa Tanzania katika mchezo wa mpira wa miguu wa ufukweni baada ya kushinda kwa mabao 6-4, lakini wamebaki na jina la Kipa Na. 1 wa timu ya Tanzania, Juma Kaseja wakisema: “Angekuwa tangu mwanzo, wangekuwa na wakati mgumu.”
Kaseja, baba wa watoto wawili ni kipa wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars pia aling'ara akiwa na Moro United, Simba, Yanga na baadaye Mbeya City.
Kaseja alikuwa kikwazo kwa Ivory Coast katika mchezo uliofanyika Jumamosi iliyopita huko jijini Abdijan ambako wenyeji walitamba kwamba wangeshinda mabao mengi, lakini kikwazo kilikuwa Kaseja na wakahoji wenyeji wa Tanzania: “Anacheza timu gani Tanzania, au mmemtoa nje ya nchi?”
“Kaseja alicheza kwa umahiri na kuzuia michomo mingi kutoka kwa washambuliaji wa Ivory Coast, na mabao aliyofungwa yalikuwa ni kwa bahati mbaya,” amesema Kocha Mkuu wa timu hiyo, John Mwansasu mara baada ya kurejea kutua jijini Dar es Salaam leo alfajiri.
Tanzania imeondolewa kwa jumla ya mabao 13-7 baada ya mchezo wa kwanza uliofanyika hapa nyumbani kupoteza kwa mabao 7-3. Michezo hiyo ni ya kuwania kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa soka la ufukweni ambako fainali zake zitafanyika jijini Lagos, Nigeria Desemba, mwaka huu.
TFF imepanga kuhakikisha kwamba inaboresha soka la ufukweni baada ya kutengeneza uwanja maalumu wa mchezo huo ulioko kando ya Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
0 COMMENTS:
Post a Comment