September 12, 2016


NA SALEH ALLY, BARCELONA

Ingawa niko mbali na nyumbani nikiendelea na majukumu mengine ya kupambana kuhakikisha wasomaji wa Championi wanapata kilicho sahihi, nimefanikiwa kuzisikia taarifa za Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye ambaye ametembelea kwenye Ofisi za Shirikisho Soka Tanzania (TFF).

Nape amefanya ziara katika ofisi za shirikisho hilo katika eneo la Karume, Ilala jijini Dar es Salaam na kujionea mambo mengi hasa yale ya kiutendaji.

Baada ya kuzuru, kiongozi huyo ametoa maagizo kadhaa katika mambo mbalimbali. Lakini hakika ningependa kujikita kwenye hili ambalo naliona limekuwa gumzo mitandaoni.

Suala la Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwenda kufanya ukaguzi katika mahesabu ya shirikisho hilo.

Nape amesema mkaguzi huyo afanye ukaguzi, jambo ambalo naona wala halina tatizo hata kidogo. Lakini utaona mjadala umekuwa mkubwa na huenda unatengenezwa ili TFF ianze kupata huruma kama vile inaonewa, jambo ambalo si sahihi.

Inawezekana kabisa, viongozi wa TFF wala hawafanyi hivyo lakini kuna wadau ambao wameamua kuwa mashabiki wa shirikisho hilo kama timu na kuamua kushabikia vitu visivyokuwa na msingi na hakika wanapoteza muda kwa makusudi.

TFF kukaguliwa na serikali, tatizo lake hasa ni lipi? Ubaya ni upi na yule anayehofia TFF kukaguliwa ana hofu kwa sababu ya jambo lipi hasa?

Je, anahisi TFF wana matatizo katika suala la matumizi? Anahisi TFF wanaonewa kwa sababu zipi hasa? Hivi kukaguliwa nako ni dhambi?

Wako wanaohoji kama TFF inaweza kukaguliwa na serikali, lakini wanashindwa kujiuliza swali dogo tu hata kabla ya kuchimba mengine kwamba shirikisho hilo ni mali ya umma.

Nimekuwa nikisisitiza suala la kuwa TFF si ya Jamal Malinzi au kiongozi yeyote wa shirikisho hilo. TFF ni mali ya Watanzania na wana haki ya kujua ambayo serikali imeanza kuyafanya sasa.

Wanaodhani TFF haiwezi kuguswa kwa kuwa mkubwa wake ni Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), wanajidanganya. TFF iko kwenye ardhi ya Tanzania, jina lake ni mali ya Watanzania. Pia viongozi walio pale hawaishi Fifa, hivyo lazima kuwe na nidhamu ya fedha na uendeshaji.

Nape apongezwe, amekuwa jasiri, amekuwa ni kiongozi ambaye licha ya kuonekana awali kama mambo ya michezo hatayaweza, lakini amekuwa akionyesha mifano mingi ambayo inathibitisha anaiweza na kwa mwendo anaokwenda nao, atapiga hatua.

Wadau wa michezo wanapaswa kumuunga mkono waziri huyo ambaye anaonyesha anataka kupambana na kubadilisha mambo ndani ya michezo ndiyo maana unaona anajitolea karibu kila siku. Leo kwenye kikapu, kuogelea, riadha na siku nyingine kaibukia kwenye soka.

Nape anaonyesha wazi anataka kuleta mabadiliko na wote tunajua kwenye michezo watu wamejimilikisha mashirikisho na vyama na kuvigeuza kuwa mali zao huku wakijua kabisa si sahihi.

Kwa anachokifanya ndani ya TFF, nacho kinaonyesha ni kutengeneza uhakika wa mambo. Jambo ambalo katika michezo na hasa soka, kimekosa nafasi kabisa.

Mambo kwenye michezo na hasa soka, yako shaghalabaghala na wote tunajua. Hivyo huu ndiyo wakati mwafaka wa kuiunga mkono serikali izidi kunyoosha mkono wake mrefu kwa ajili ya kutengeneza nidhamu na baadaye ujenzi upya uanze.

Tuache kuwa watu wa kulaumu kwa kuwa maslahi yetu yameguswa. Tuache kuwa wafuata mkumbo kwa kuelezwa kitu tu na kuanza kukurupuka huku tukiamini eti TFF inaonewa.

Kila unachoelezwa, vizuri kutafakari. Tumuunge mkono Nape pamoja na serikali katika uletaji mabadiliko. Waungwana, nyumbani michezo imekufa kabisa na uongozi duni ni namba moja.

Kwa kuwa sasa tumepata serikali ambayo hailali, basi tuiunge mkono na tuepuke kuingia kwenye mitego ambayo inakuwa kwa maslahi ya wachache.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic