September 16, 2016

Na Saleh Ally, Barcelona
Beki wa zamani wa FC Barcelona, Eric Sylvain Abidal ni kati ya wanasoka maarufu hapa Hispania, lakini ni maarufu dunia nzima kutokana na mafanikio makubwa aliyoyapata akiwa mwanasoka.

Ni maarufu kwa kuwa mafanikio ni makubwa, alichukua taji la Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ mara nne akiwa na Barcelona, Copa de Rey mara mbili, Ligi ya Mabingwa, Uefa Super Cup, zote mara mbili kama ilivyokuwa ubingwa wa dunia wa klabu.

Achana na hivyo, amebeba Ligi ya Mabingwa mara mbili, mara moja akiwa na kumbukumbu ya kuliinua kombe baada ya kukabidhiwa. Nahodha wa Barcelona wakati huo, Cares Puyol, alimkabidhi unahodha ili alibebe ikiwa ni kuonyesha upendo kwake kutokana na kupatikana na ugonjwa wa ini.

Ubingwa wa nchi, Hispania haikuwa mara ya kwanza. Akiwa na Lyon kwao Ufaransa aliiongoza timu hiyo kubeba ubingwa wa Ligue 1 mara tatu.

Unapozungumzia mafanikio, kwa Abidal haliwezi kuwa jambo geni au la kushangaza. Beki huyo wa pembeni alijulikana kutokana na kasi, uwezo mkubwa wa kupanda na kupiga krosi na akarejea kuzuia.





Tangu 2007 hadi 2013, aliitumikia Barcelona kwa mafanikio makubwa akiichezea mechi 125 chini ya makocha wawili tofauti. Kwanza ni Pep Guardiola halafu Tito Vilanova ambaye sasa ni marehemu.

Sasa ni mstaafu akiwa na umri wa miaka 37, bado anaendelea kuishi katika Jiji la Barcelona akiendelea na maisha yake. Huku akifanya kazi katika taasisi yake isiyo ya kiserikali ya Eric22 Abidal Foundation.

Kazi kubwa ya taasisi yake ni kusaidia watoto wenye matatizo ya ini pamoja na kansa, ugonjwa ambao aligundulika kuwa nao Machi 15, 2011 na kusababisha kuanza kuyumba kwa utendaji wake uwanjani.

Ingawa alifanikiwa kurejea uwanjani na kuisaidia Barcelona. Abidal anaamini ugonjwa huo ulichangia kumuondoa mapema lakini hajawahi kumlaumu Mwenyezi Mungu huku akisisitiza, kwa Mwislamu, kila kitu ni vizuri kushukuru.

Katika mahojiano maalum na gazeti hili jijini hapa, Abidal anasema atabaki Barcelona ikiwezekana maisha yake yote kwa kuwa ndiyo kumekuwa nyumbani na sehemu ambayo inafanya akumbuke mambo mengi sana.

“Baada ya kuondoka Barcelona nilikwenda Monaco ambako nilikulia kisoka, baadaye nikaenda Olimpiakos kabla ya kustaafu lakini Barcelona ni kitu kilicho ndani ya moyo wangu. 
“Kwanza familia yangu, inaamini hapa ndiyo nyumbani,” anasema Abidal ambaye ni baba wa mabinti wawili Meliana na Camelia, mkewe ni mwanamichezo pia kwa kuwa ni mcheza sarakasi, anaitwa Hayet Kebir.

“Lakini wakati nilipopata matatizo ya ugonjwa wa ini, nilionyeshwa kwamba mimi ni mwanafamilia wa hapa. Watu walinionyesha upendo wa juu sana.

Barcelona walinionyesha mimi ni mtu, nastahili mapenzi na sikuacha kulia kila kukicha. Hivyo siwezi kusahau, hapa ni nyumbani,” anasema.

Ofisi ya Abidal, ipo katikati kabisa ya Jiji la Barcelona. Umbali wa kilomita mbili na nusu kutoka ulipo Uwanja wa Camp Nou unaomilikiwa na Barcelona.

Amekuwa akifanya kazi zake, kuendelea kuwasaidia watu mbalimbali barani Ulaya na Afrika na zaidi ni watoto wadogo.

Kuwa nje ya mpira, hakumfanyi kuacha kusahau matukio kadhaa ambayo anasema yanaendelea kubaki kwenye kumbukumbu ya maisha yake.



Unaona hapa ofisini, karibu kila kitu kinaonyesha soka. Hata runinga sasa ni soka (anaonyesha TV ambayo imewekwa kwenye chaneli ya Barca TV, huku yakionyeshwa mabao 10 Bora ya Messi ya Ligi ya Mabingwa). Rafiki zangu wengi ni wanasoka, hivyo siwezi kusahau matukio ya kwenye soka.

“Yako mengi, ya zamani na hata sasa, bado yanaendelea kutokea lakini lile la kupewa unahodha na Puyol kwa niaba ya wachezaji wengine wa kikosi cha Barcelona mwaka 2011 pale London, wakati mwingine linanikumbusha, nasikia furaha au majonzi,” anasema.

Ilikuwa Mei 28, 2011 mbele ya watazamaji 85,000 kwenye Uwanja wa Wembley, London. Puyol alivua kitambaa cha unahodha na kumkabidhi Abidal baada ya Barcelona kuitundika Manchester United mabao 3-1 katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Abidal anasema anayakumbuka mambo mengi sana. Mfano tukio la mashabiki kumpigia makofi kwa sekunde 22, kuonyesha mapenzi kwake kwa kuwa alikuwa akivaa namba 22. Kama hiyo haitoshi ni uamuzi wa Dani Alves kuamua kumpa upande mmoja wa ini lake ili apate matibabu.

Kama hiyo haitoshi, alishangiliwa na kuonyeshwa kwenye ubao kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu, jambo ambalo si rahisi kutokea.


Fuatilia kwenye gazeti hili kesho Jumamosi pamoja na kwenye SALEH JEMBE kujua anasemaje kuhusiana na mambo hayo na yalivyomtokea.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic