October 3, 2016



Na Saleh Ally
NILIWAHI kuelezea kuhusiana na namna kiungo Jonas Mkude alivyobadilika na kuanza kuwa mtu tofauti baada ya kuingia mkataba mpya na Simba ambao uligharimu zaidi ya Sh milioni 40.

Mkude alikuwa akionekana karibu kila sehemu ya starehe, wakati mwingine akiwa amevua shati na kuzunguka huku na huko kwenye sehemu za vinywaji au baa, ilimradi tu.

Watu wengi wakalaumu sana, kama ilivyo kawaida ya watu wanaokosa hoja za msingi. Wakaanza kulalama kwamba ninamsakama huku wakisema mimi ni shabiki wa Yanga au vinginevyo, nikapuuzia huo upuuzi.

Ninachoshukuru, Mkude alinielewa na kubadilika na baada ya hapo nikafuatilia mwenendo wake kwa miezi kadhaa na mwisho nikampongeza, hakuna ubishi hadi sasa anafanya kazi yake vizuri.


Safari ya pili, niligeuza jicho langu zaidi niliangalia kwa Hassan Isihaka ambaye alipewa unahodha wa Simba, jambo ambalo nililiona kichekesho na nikawa wazi kabisa kwamba hakustahili hata kidogo.

Isihaka hakuwa kiongozi uwanjani, hakujua hata kuizungumzia timu yake inapofikia anahojiwa. Niliwaeleza ukubwa wa Simba na uamuzi usio sahihi wa kumchagua Isihaka kuwa nahodha. Wako pia waliosema ninamsakama na vinginevyo, nikapuuzia upuuzi huo pia.

Baadaye Simba walifanya mabadiliko na wengine wakakubali, kweli ukubwa wa Simba ulimuelemea Isihaka na makocha wakaona hata nafasi ya kucheza alikuwa akiwahishwa. Ninaamini aliko, atakuwa anajifunza na huenda siku moja atarejea Simba au kwenda kwingine akiwa beki bora.


Safari hii ninarejea kwa Mkude tena, ninazungumzia suala la cheo cha unahodha ambacho anashikilia. Yeye ndiye kiongozi wa Simba ndani ya uwanja.

Unapopewa jukumu la kuiongoza timu kama Simba, pia kumbuka ni jahazi kubwa na kongwe lenye historia yenye rekodi lukuki. Hivyo Mkude amepewa kazi ngumu  na lazima aonyeshe ni nahodha hasa.

Kadi nyekundu aliyopewa katika mechi dhidi ya Yanga ni ya kipuuzi na inaonyesha bado hajapevuka vizuri na mambo mawili yanaweza kufuata baada ya hapo.

Moja, ajifunze na kubadilika na kama hatabadilika basi hakuna ubishi hatakuwa kwenye kundi la wanaostahili kuwa manahodha wa Simba.

Nahodha ni kiongozi, kwenye matatizo ndiye anafanya kazi ya kuwatuliza wenzake badala ya kuwa kiongozi wa ugomvi, kiongozi wa kuchanganyikiwa au kiongozi wa kusaidia kuwatoa wenzake kwenye msitari kwa kuwa ameshindwa kuzuia hasira zake.

Mwamuzi Martin Saanya aliiminya Simba na kufanya kosa la kipuuzi. Amissi Tambwe hakufanya ajizi, akafunga bao kwa ufundi wa juu kabisa tayari Simba ikiwa nyuma kwa bao moja.


Wakati hali hiyo inatokea unategemea kumuona nahodha sahihi anakuwa mtu anayewaongoza wenzake kuondoka kwenye matatizo zaidi ikiwezekana kuwaondoa na yeye azungumze na mwamuzi kutokana na kosa alilolifanya.

Nahodha anaweza kuzungumza na mwamuzi kwa maneno ambayo angeelezwa zaidi kuliko kumsukuma, kama Mkude alivyomsukuma Saanya hadi chini. Halikuwa jambo sahihi na linamuingiza yeye kama sehemu ya kosa na hakuna anayeweza kusema hakutarajia kupata kadi nyekundu. 

Unapomsukuma mchezaji mwenzako akaanguka, ujue kadi inafuatia, sasa jiulize kwa mwamuzi inakuwaje?
Mkude alijua kosa lake litazaa kadi nyekundu, lakini jiulize kwa nini atalifanya? Ikiwa jibu ni hasira, vipi kiongozi atawaliwe na hasira kuliko anayewaongoza! Unafikiri ikiwa hivyo kutakalika kweli?

Ndiyo maana nilisema leo narejea tena kwa Mkude, wakati mwingine ambao anatakiwa kujifunza zaidi na kujua thamani ya kitambaa cha unahodha katika mkono wake wa kushoto kuwa ni kofia kubwa na anatakiwa kuiheshimu, kuithamini na kuitumia sahihi kwa heshima na mafanikio ya timu yake.








7 COMMENTS:

  1. "Amissi Tambwe hakufanya ajizi, akafunga bao kwa ufundi wa juu kabisa tayari Simba ikiwa nyuma kwa bao moja." Kuna ufundi gani pale? Na makosa ya refa haikuwa tu kuachia goli ambalo sio halali bali pia kukataa goli halali la kiufundi la Ajibu ambalo hujalitaja. Mi naona hasira za Mkude zilikuwa ni mlundikano wa mwenendo mzima wa mchezo na sio hilo kosa moja tu. Nadhani upunguze unazi wa kusifia ufundi wa kushika na mikono. Angekuwa fundi ange control mpira na sio kushika na mikono. Ulitakiwa kumkosoa maana kushika kwake kumemkosesha goli halali kukampatia goli haramu na kumpa sifa mbaya mbele ya wapenda haki kwenye soka.

    ReplyDelete
  2. Tatizo lako bw Salehe unatazama upande mmoja, ungekemea goli na maamuzi ya refa kabla ya kadi ungefaa sana. Kumbuka historia ni dawa na ni mwalimu. Wewe mwenyewe ulisema refa aliye boronga mechi ya Costal na Yanga akafungiwa apewewa mechi ngumu ya watani wa jadi! Huyu Saanya aliwahi kumpa kadi ya njano Kanavaro akiwa ana mshauri kama kepteni. Saanya ana mambo nyuma yake.

    ReplyDelete
  3. Tatizo lako bw Salehe unatazama upande mmoja, ungekemea goli na maamuzi ya refa kabla ya kadi ungefaa sana. Kumbuka historia ni dawa na ni mwalimu. Wewe mwenyewe ulisema refa aliye boronga mechi ya Costal na Yanga akafungiwa apewewa mechi ngumu ya watani wa jadi! Huyu Saanya aliwahi kumpa kadi ya njano Kanavaro akiwa ana mshauri kama kepteni. Saanya ana mambo nyuma yake.

    ReplyDelete
  4. Kaka unachambua vizuri lakini swala LA kadi nyekundu la mkude nakupinga kidogo kwa sababu yule ni captain wa timu na tunavyojua mechi kama ile presha ya wachezaji na refa na timu yake huwa juu mkude alikuwa sahihi kabisa kudai haki yake na kuwa haya mambo sio mara Moja kutokea upande wa simba

    ReplyDelete
  5. Salehe sijakuina ukiongea goli alokataaaa mwamuzi saanya lile la ajib ile ni offside ya wapi hilo koja na pili mkude hakumsukuma mwamuzi bali alijikwaa kwa ajib tatu ww tulicheza wote mpira sana tena nakumbuka hata wewe ulikua na hasira kwenye maamuzi mabovu ya vijimechi vyetu vya mtaaani.mimi oia uwanjani nilikuwwpo na niliona kwa hili usimuonee mkide nimeona habar yako wewe ni yanga wa kutuowa tia maelezo usilete ushabiki saleh.hujaonhelea kabisa lile goli ambalo walisema ni offside nilitegemea utalauku viongozi wa tff kwa kumpa achezeshe wakat alikua amefungiwa badala yake unakuja kumlaumu mkude.washabiki wenyewe yulikasirika kwanini asikasirike mkude??Yafiche mapenzi yako kwenye kuandika habar uwe unabalance.refa kakataaa goli la simba la wazi kaja kukibali mtu kashika unategemea nini na ile ni mechi kubwa???nakuamini sana wewe ni mwabahabar mzuri ila kwa hili umenishangaza kaka.

    ReplyDelete
  6. Salehe sijakuina ukiongea goli alokataaaa mwamuzi saanya lile la ajib ile ni offside ya wapi hilo koja na pili mkude hakumsukuma mwamuzi bali alijikwaa kwa ajib tatu ww tulicheza wote mpira sana tena nakumbuka hata wewe ulikua na hasira kwenye maamuzi mabovu ya vijimechi vyetu vya mtaaani.mimi oia uwanjani nilikuwwpo na niliona kwa hili usimuonee mkide nimeona habar yako wewe ni yanga wa kutuowa tia maelezo usilete ushabiki saleh.hujaonhelea kabisa lile goli ambalo walisema ni offside nilitegemea utalauku viongozi wa tff kwa kumpa achezeshe wakat alikua amefungiwa badala yake unakuja kumlaumu mkude.washabiki wenyewe yulikasirika kwanini asikasirike mkude??Yafiche mapenzi yako kwenye kuandika habar uwe unabalance.refa kakataaa goli la simba la wazi kaja kukibali mtu kashika unategemea nini na ile ni mechi kubwa???nakuamini sana wewe ni mwabahabar mzuri ila kwa hili umenishangaza kaka.

    ReplyDelete
  7. salehe unatakiwa kujua, mkude sio nahodha wa kwanza kutolewa na kadi nyekundu kwa kupandwa na hasira, kumbuka yule ni binadamu, na refa alilundika makosa mengi mno ambayo pengine ungekuwa hata wewe ungefanya hivyohivyo...unakumbuka kisa na zidane world cup ujeruman?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic