October 28, 2016Yanga ilipata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya JKT Ruvu, juzi Jumatano lakini aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Hans van Pluijm alihusika katika ushindi huo lakini zaidi ni jinsi mashabiki wa timu yake wakiongozwa na shabiki maarufu, Mama Yanga walivyompokea kwa furaha ikiwemo kuzuia gari lake wakati akitoka kushuhudia mchezo huo.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar, Pluijm alikuwepo uwanjani hapo akifuatilia mechi hiyo, aliwasili saa tisa alasiri akiwa kwenye gari aina ya Toyota Harrier.


Mara baada ya mechi hiyo kumalizika, wakati akiondoka uwanjani hapo, Pluijm alivamiwa kwenye gari lake na kundi la mashabiki waliomtaka afungue vioo na kuagana nao, uamuzi ambao aliufanya kwa kushusha kioo.

Baada ya kushusha kioo mashabiki waliongezeka na wengine wakamtaka ashuke lakini alichofanya ni kufungua mlango wa gari hilo na kusalimiana nao huku wengine wakipiga picha akiwemo muigizaji wa filamu, Dokii ambaye ni shabiki mkubwa wa Yanga.


Wakati hayo yakitokea, baadhi ya mashabiki walikuwa wakilalamika kitendo cha uongozi wa Yanga kusababisha kocha huyo kujiuzulu wakati amedumu muda mrefu kikosini na bado hajaonyesha kupoteza mwelekeo.

Awali, wakati akifuatilia mchezo huo, Pluijm alikuwa makini muda wote na kuandika baadhi ya vitu kadhaa kwenye kitabu chake kama alivyokuwa akifanya alipokuwa kocha wa timu hiyo.

Aidha, alikuwa akiwasiliana na kiongozi mmoja wa benchi la ufundi la Yanga ambapo ilionekana akitoa maelekezo.

Pluijm alishindwa kuzuia hisia zake kwa kunyanyuka kushangilia bao la Obrey Chirwa na mengine yaliyofungwa.

Baada ya mechi hiyo, Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema kuondoka kwa Pluijm ni pengo kwao lakini hawataacha kupambana ili kupata ushindi kwenye mechi zao zijazo na kudai kuwa hata ushindi huo umechangiwa kwa kiasi kikubwa na mafunzo ya Pluijm aliyokuwa akiyatoa kikosini hapo.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV