KASI kubwa ya kuzifumania nyavu ambayo mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga raia wa Zambia, Obrey Chirwa ameanza kuionyesha hivi karibuni katika michuano ya Ligi Kuu Bara imewafanya wale waliokuwa wakimpuuza awali kuwa hana lolote kufuta kauli zao na kuanza kumuombea mema kwa Mungu.
Mmoja kati ya watu hao ni Mzee Ibrahim Akilimali ambaye siku chache baada ya Chirwa kutua nchini alianza kumponda kuwa hana lolote na kiwango chake siyo cha kuitumikia timu hiyo, hivyo Yanga imepoteza fedha zake kwa kumsajili.
Hata hivyo, mzee Akilimali alifuta kauli zake hizo alizokuwa akizitoa kwa Chirwa baada ya kusema kuwa alikuwa akifanya hivyo kwa lengo ya kumjenga ili aongeze bidii uwanjani.
Alisema kwa sasa anafurahishwa na kiwango cha mshambuliaji huyo, kwani hivyo ndivyo alivyokuwa akitaka afanye kwa faida ya timu ambayo ilimsajili kwa mamilioni ya fedha kuliko mchezaji mwingine yeyote klabuni hapo.
“Ujue watu walikuwa wananielewa vibaya lakini lengo langu lilikuwa ni kumfanya aongeze bidii na sikuwa na nia nyingine dhidi yake.
“Lakini kwa sababu ameanza kufanya kazi tuliyokuwa tukiikusudia kutoka kwake, sina tena tatizo naye na sasa namuombea kwa Mungu aendelee kufanya vizuri, kama kulikuwa na watu wamemfunga miguu basi washindwe,” alisema Akilimali.
Mpaka sasa, Chirwa amefunga mabao matano kwenye mechi nne alizoanza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
0 COMMENTS:
Post a Comment