October 12, 2016Hatimaye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) imeanza kuichunguza akaunti ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kama ilivyoagizwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye katika taarifa yake iliyotolewa hivi karibuni ili kubaini madudu yanayofanyika.

Aidha, Nape aliamua kufikia maamuzi hayo kufuatia kupewa taarifa kupitia kwa wadau mbalimbali kutakiwa kuichunguza akaunti hiyo ya TFF jambo ambalo aliamua kulifanyia kazi kwa kuiagiza Takukuru kuanza kazi yake ikiwa ni pamoja na kufuatilia chaguzi mbalimbali zinazoendelea kufanyika hivi sasa mikoani hadi itakapofika ngazi ya TFF katika uchaguzi mkuu wa rais utakaofanyika hapo mwakani.

Ofisa Habari wa Takukuru, Mussa Msalaba, ameibuka na kusema kuwa, tayari wameshaanza kutekeleza agizo hilo la Waziri Nape, ambapo wameanza kufanya uchunguzi TFF kimyakimya.

“Tayari tumeshaanza kufanya uchunguzi wetu wa awali na tumeanza kwa kuchunguza akaunti za TFF pamoja na masuala mbalimbali yanayohusu shirikisho hilo, japokuwa tunafanya kimyakimya na kwa upande wetu wenyewe tunajua tunafanyaje kazi yetu, siyo lazima kwa upande wao wafahamu nini kinaendelea na tunachokihitaji sisi ni kubaini kilekile tulichotakiwa kufanya.

“Tumeanza kazi hiyo katika mikoa yote kwenye chaguzi za mikoa na wilaya zinazofanyika hivi sasa lakini tunakutana na ugumu wa hali ya juu kwa kuwa suala hili watu huwa wanapeana vichochoroni au chooni lakini sisi kama Takukuru hatutashindwa kitu na tunaendelea kufanya kazi yetu kama tulivyopangiwa.


“Na kwa upande wa suala la Rais wa Simba, Evans Aveva, bado mchakato unaendelea kwa kufanya uchunguzi kwa kuwa suala lao ni pana, hivyo linahitaji muda zaidi kabla ya kuliweka wazi,” alisema Msalaba.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV