October 12, 2016Uongozi wa Klabu ya Azam umesema kuwa pamoja na kwamba wanacheza leo dhidi ya Stand lakini watautumia mchezo huo kama sehemu ya maandalizi yao kabla ya kuwavaa Yanga wikiendi hii.

Azam inayonolewa na Mhispania, Zeben Hernandez, leo Jumatano itakuwa na kibarua kigumu cha kumenyana na Stand United iliyo katika nafasi ya pili kwenye msimamo katika mchezo wa ligi ambao utapigwa kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Msemaji wa Azam, Jaffar Idd alisema licha ya kwamba wanafikiria pointi za Stand lakini mawazo yao yapo kwa Yanga kutokana na timu hiyo kuwa ndiyo wapinzani wao wakubwa kwa sasa.

“Mechi hii na Stand ina umuhimu wake kama zilivyo mechi nyingine ambapo lengo letu ni kupata pointi tatu ambazo zitatukomboa hapa tulipo lakini tunawafikiria zaidi Yanga ambao tutacheza nao wikiendi hii kwa sababu wao ni wapinzani wetu wa karibu ukilinganisha na timu nyingine.

“Hata kocha Zeben mipango yake ameielekeza kwenye mechi na Yanga kwa sababu hiyo ni kubwa na muhimu zaidi ukilinganisha na hii kutokana na historia yetu ilivyo kwa sasa na pia sisi tunataka kuendeleza kutopoteza mbele yao kama tulivyofanikisha kuwafunga mwanzoni mwa ligi,” alisema Idd.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV