November 2, 2016

Na Saleh Ally
Misimu miwili imepita, mshambuliaji kinda wa Simba, Ibrahim Ajibu Migomba alianza kuonekana na baadaye akawa msaada kwenye kikosi cha Msimbazi.

Ajibu ni mchezaji mwenye kipaji hasa, mchezaji ambaye baadaye anaweza kuwa tegemeo katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kama ataamua.

Ninasema akiamua kwa kuwa kipaji alichonacho, kimezidiwa nguvu na yeye alivyo. Kiingereza kuna talent na character, yaani kipaji na kasumba. Hivi vinategemeana.

Mchezaji anaweza akawa na kipaji sana, lakini kasumba ikamuangusha, akashindwa kwenda mbali na kufanikiwa. Ajibu anaangushwa na kasumba, maana inaonekana ni mtu asiyejali wala asiyeangalia nyuma.

Ajibu haangalii miaka minne tu iliyopita hakuwa akijulikana, hakuwa tegemeo Simba wala hakuwa gumzo popote katika mpira wa Tanzania. Lakini kwa namna alipofikia sasa, anaonekana kama anaona ndiyo amefika mwisho au hakuna kama yeye.

Uchezaji wa Ajibu ni mchezaji anayeweza kucheza anavyotaka, maji kupwa maji kujaa. Leo vizuri, kesho hovyo kabisa. Yaani hajali, itakavyokuwa siku ndiyo ilivyo, hawezi kuibadilisha kwa kuibadilisha kwa kutaka kusimamia usahihi.

Ndani ya kikosi cha Simba, ukichunguza kama ni mfuatiliaji wa muda mwingi bila ya kuchoka, utagundua wastani wa msaada na mzigo, Ajibu anaweza akawa mzigo zaidi ya msaada ndani ya Simba.

Si mchezaji anayekaba kwa juhudi sana, si mchezaji anayejali sana. Mara nyingi ‘move’ za Simba zinafia kwake anapopoteza mpira na hasumbuki sana.

Lakini ni mchezaji ambaye anacheza zaidi na jukwaa kuliko wachezaji wote wa Simba. Anataka kuonekana yeye, si timu nzima. Anataka kujifurahisha yeye, si kuwafurahisha mashabiki kwa kuihakikishia timu ushindi.

Hauwezi kuwa mchezaji unayetaka kucheza kwa juhudi siku unayotaka tu, hauwezi kuwa mchezaji unayetaka kujifurahisha wewe tu huku ukijua si sahihi.

Mbaya zaidi, Simba nao hakuna anayeweza kumueleza kwa kumuweka chini kwamba Tanzania ni nchi kubwa sana, ina vijana wengi wenye vipaji na wako walio makini wanataka maendeleo. Hivyo nafasi yake aliyoipata Simba ni adimu na wengi wanaililia, wakiipata hawataifanyia mchezo kama anavyofanya yeye.

Angalia presha aliyonayo Ajibu baada ya Kocha Joseph Omog alipoanza kumtumia kijana mwingine Mohamed Ibrahim maarufu kama Mo Ibrahim.

Huyu anacheza direct football, yaani mpira wenye malengo na anacheza kwa ajili ya ushindi. Anacheza kwa ajili ya timu na mafanikio. Ajibu amekuwa akitokea benchi na lazima kichwa kimuume.

Huu ndiyo wakati kwake wa kuchagua kusuka au kunyoa, acheze mpira wenye manufaa kwa ajili ya klabu yake, au aendelee na shoo zisizokuwa na msingi, mwisho Mo Ibrahim na wengine walio makini wazidi kupasua anga.

Kawaida katika maisha, ukipata nafasi na uwezo unao, basi fanya kweli. Pia unapaswa kuamini wenye uwezo ni wengi lakini nafasi ni chache. Kuendelea kuichezea, siku ikigeuka basi, ujue kuna kazi ngumu.

 Muangalie Mo Ibrahim anavyocheza, angalia anavyofanya kazi anapokuwa na mpira, mchunguze Simba inapokuwa imepoteza mpira. Maana yake kwa kocha makini kama Omog, lazima atoe nafasi zaidi kwake kuliko Ajibu ambaye anachukulia pa.

Watanzania wengi tunaona aibu kuambiana, lakini ninachokiandika leo najua wengi wamekiona wakiwemo viongozi wa Simba, lakini wasingependa kumuudhi Ajibu, maana si vema kumkasirisha.

Mimi kwa makusudi kabisa nikiwa nimelenga, ninamkasirisha na kumueleza aache nalenale, awe makini na hakuna mafanikio kwa watu wasio makini na kile wanachokitumikia.

Kwa maana ya kipaji, Ajibu ana nafasi kubwa ya kufanya vizuri zaidi ikiwezekana kuliko vijana wengi sana hapa nchini katika michezo. Lakini lazima abadilike na aone umakini, kulenga na kujenga malengo yanayolenga mafanikio, ndiyo itakuwa njia sahihi ya yeye kutoka. Kufika Simba, hakuwezi kuwa mwisho wa safari ya mafanikio ya mchezaji.0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV