Beki wa Yanga, Vincent Bossou ameweka bayana kwamba hawakuwa na wasiwasi na mwendo wa Simba walivyoanza Ligi Kuu Bara kwa nguvu kubwa kwani walitambua itafika kipindi pumzi hiyo itakata na watajikuta wakirejea chini kama ambavyo inawakuta sasa kwenye mechi zao mbili zilizopita.
Simba inayonolewa na Mcameroon, Joseph Omog kwenye mechi zake 13 za mwanzo ilianza kwa ushindi kabla ya kupoteza mechi zake mbili za mwisho dhidi ya African Lyon na Prisons ambapo hata hivyo bado wanaongoza ligi wakiwa na pointi 35.
Bossou aliye na kikosi cha timu ya taifa ya Togo nchini Tunisia amesema kuwa hawakuwa na wasiwasi wowote juu ya kutetea ubingwa wao kwa msimu huu licha ya Simba kuwa kileleni kwa sababu waliona kiwango walichoanza nacho kingekwama njiani kwa sababu ya uchovu unaosababishwa na kutumia nguvu nyingi katika mechi zao.
“Tulijuwa kuwa Simba lazime waje kufanya vibaya kwa sababu walianza kwa nguvu kubwa sana na kukamia mechi zao ambapo madhara yake mwishoni wamejikuta wakifungwa kirahisi kwa sababu wachezaji tayari wameshachoka kwa sababu wametumia nguvu kubwa.
“Sasa baada ya wao kuyumba huu ni muda wetu wa kuhakikisha tunafanya vizuri na tuna uhakika wakufanya hivyo kwa sababu kila mechi kwetu tunachukulia kama fainali na tunacheza kwa kujituma kupata pointi tatu,” alisema Bossou.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment