November 18, 2016

BAADHI YA VIONGOZI WA SIMBA AMBAO WAMEKUWA WAKIHUSIKA NA SUALA LA USAJILI.


Na Saleh Ally
SIKU tatu sasa tangu dirisha la usajili lifunguliwe, tayari timu mbalimbali zimeanza kufanya usajili kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.

Mzunguko huo wa pili utakuwa na mechi 15 kwa kila timu lakini hakuna anayeweza kukataa kwamba utakuwa ni mgumu kwelikweli.

Kazi itakuwa ngumu kwa kuwa kila timu itakuwa inawania inachokitaka. Inaonekana si zaidi ya timu nne zitakuwa zinawania kutwaa ubingwa.

Lakini kutakuwa na zaidi ya timu 10 zitakazokuwa zikiwania kubaki katika Ligi Kuu Bara kwa hofu ya kuteremka daraja, hivyo hali hiyo itaongeza ugumu na hakika timu zitakazofaidika ni zile zitakazofanya mabadiliko katika suala la usajili wa dirisha dogo.

Kila timu imeona kile inachotakiwa kufanya baada ya kuwa imecheza mechi 15 za mzunguko wa kwanza. Kila upande umeona faida na hasara na kile ambacho wanachokifanya. Simba ilifaidika kwa kumaliza ikiwa na tofauti ya pointi mbili na Yanga aliye nafasi ya pili.

Simba imeona kuwa ilimaliza mzunguko wa kwanza ikiwa na bahati mbaya kuu. Kwa kuwa mechi mbili za mwisho ilipoteza zote, maana yake pointi sita zikaenda na maji.

Kweli Simba inaongoza ligi, lakini matarajio sahihi yanaonyesha Simba haikupaswa kumaliza ligi ikiwa imepunguza kwa kiasi kikubwa pengo la pointi kwa kuwa lilikuwa nane, mwisho limekuwa pointi mbili tu.

Kutokana na hali inavyokwenda, naingia hofu kama mambo yanakwenda kitaalamu kwa kuwa kuna mambo mengi yamechanganyika kama jazba, mihemko na matakwa binafsi ya baadhi ya watu mbalimbali.

Wako viongozi ambao wameonyesha wazi kutofurahia mwenendo wa mzunguko wa kwanza wa timu zao.

Wako ambao hawakupenda kuonekana kibonde, wangependa kujirekebisha. Pia wako ambao wanaona kwenye timu zao kuna matatizo, mfano hujuma au kuangushwa na wachezaji hivyo wangependa wanaowaona ni tatizo waondoke.

Kawaida, wakati wa usajili ni wakati ambao unahusisha utaalamu zaidi. Si suala la kutimiza hisia za mwenyekiti wa usajili, mjumbe wa kamati ya usajili au kiongozi wa klabu ambaye hampendi mchezaji fulani.

Kama mtaacha hisia zichukue nafasi kuliko uhalisia, basi usajili utakuwa si sahihi, si ule ambao unaweza kusaidia mambo na badala yake nafsi za wachache na mwisho mambo yataharibika.

Iwapo kuna kiongozi hakufurahishwa na mchezaji fulani, basi hapaswi kutanguliza hisia zake za hasira au mihemko na kutaka kuona mchezaji huyo lazima anaondoka kwenye klabu husika.

Badala yake afuate utaratibu na vizuri kukubaliana pia kwamba mtu anayehusika kabisa na masuala ya usajili ni bosi wa benchi la ufundi ambaye ni kocha. Huyu ndiye anayepaswa kusema kinachotakiwa kufanyika kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chake.

Aachiwe kocha kwa kuwa ndiye aliyekiongoza kikosi na amejua matatizo au kitu chenye upungufu na angepaswa kuziba au kupunguza vipi.

Ripoti ya kocha ambayo anakuwa amesaidiana na timu ya ufundi ndiyo itakuwa na mwongozo sahihi wa nini kifanyike kwa ajili ya kikosi chake na ubora utakuwa sahihi kuliko kila mmoja kuingilia.

Wakati mnaheshimu hiyo ripoti ya kocha, pia mnapaswa kupunguza papara kwa kuwa muda unaruhusu kwa mwezi mzima hadi Desemba 15.

Kuwahi inaweza kuwa vizuri lakini kufanya mambo kwa uhakika huku mkiupisha muda pia ni jambo bora na sahihi.


Kwa kifupi suala hili la usajili halihitaji papara kwa kila upande. Kuanzia kwa viongozi kuepusha mihemko pia, lakini katika usajili si kukurupuka tu kwa kupata ujiko, mmemsajili mchezaji wa timu fulani.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV