Kazi bado ngumu, unaweza kusema hakijaeleweka kuhusiana na suala la beki Hassan Kessy baada ya Yanga na Simba kukutana leo.
Pande hizo mbili zimekutana bila ya aliyetakiwa kuwa msuluhishi, Said El Maamry ambaye ni mjumbe wa heshima wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Lakini mwisho, Simba imetaka kulipwa kuanzia kati ya Sh milioni 100 hadi 200 na Yanga wameenda kulijadili.
Taarifa za ndani kutoka katika kikao hicho zimeeleza, kuwa Simba walianzia Sh milioni 500 wakiondoa dau lao la zaidi ya Sh bilioni moja.
"Kweli, mwisho Simba wamesema wanaweza kulijadili tena katika ofa kuanzia Sh milioni mia hadi mia mbili.
"Awali Yanga walisema wako tayari kutoa Sh milioni kumi, lakini Simba wakakataa katakata," kilieleza chanzo.
Katika kikao hicho, Simba iliwakilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe, wakati Yanga iliwakilishwa na mjumbe mmoja wa kamati ya utendaji, wanasheria wawili na Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit ambao hata hivyo mara kadhaa walilazimika kutoka nje na kuzungumza na simu.
Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, iliwataka Simba na Yanga kukutana na kulimaliza suala hilo kabla ya yenyewe kutangaza uamuzi wake.
0 COMMENTS:
Post a Comment