November 18, 2016


Na Saleh Ally
DIRISHA dogo la usajili limeshafunguliwa na sasa gumzo limeanza kila upande ukiamini fulani anatua timu fulani au anaondoka sehemu fulani.

Hiki ndiyo kipindi kila mtu ana uwezo wa kueleza jambo lake analolijua yeye kulingana na tetesi au hali halisi.

Moja ya mazungumzo ni kurejea kwa mshambuliaji Emmanuel Okwi, ambaye inaelezwa anatakiwa kujiunga na Simba akitokea Denmark ambako aliuzwa na Simba katika klabu hiyo ya SonderjysjkE.

SALEHJEMBE imeefunga safari hadi kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe ili kupata uhakika wa kila jambo, kwamba nani anaachwa na nani anachukuliwa. Lakini vipi kuhusiana na Okwi?

SALEHJEMBE: Umeuonaje mzunguko wa kwanza ambao umemalizika mkiwa kileleni lakini mmewashangaza wengi kwa kupoteza pointi sita katika mechi mbili tu za mwisho?
Hans Poppe: Tulianza vizuri sana na tulijitahidi kuongoza hadi kwa pengo la pointi nane. Mwisho wetu haukuwa mzuri sana kwa kweli, inawezekana kwa makosa yasiyo ya kawaida.

SALEHJEMBE:  Makosa yasiyo ya kawaida, unaweza kulifafanua vizuri hilo?
Hans Poppe:  Mchezaji unamjua, unajua uchezaji wake alivyo lakini katika mechi moja, mbili anabadilika na kucheza katika hali ambayo inashangaza kabisa.

SALEHJEMBE:  Hivyo hofu yako hapo ni nini, kama unazunguka kidogo?
Hans Poppe: Hofu inaweza kujumuisha mambo mengi, kwamba huenda ni uchovu, umri, kukosa uzoefu, ugonjwa au pia kwa makusudi kwa maslahi yake. Haya mambo ya watu kutumika yapo, lakini naweza kusema ni hisia na tunapaswa kuyafanyia kazi na mwisho tujue, kama kuna ukweli basi tutachukua hatua kwa kuwa tukiyaacha, katika mzunguko wa pili, yatatuumiza.

SALEHJEMBE: Kwa nini muwe na hofu sana wakati mwanzo mlianza vizuri, hamuamini katika makosa?
Hans Poppe: Makosa yapo, ndiyo maana nakuambia tutafanya uchunguzi. Tunaamini pia kuna wale waliotudharau wakiamini nguvu ya soda, sasa wameona tunazidi tu kusonga mbele, wanaweza wakawa wameamua kuingia na kutuharibia kwa makusudi. Haya mambo yapo na yametukwamisha kwa misimu minne sasa.

SALEHJEMBE: Okwi anakuja, labda ni lini?
Hans Poppe: Nimesikia sana mtandaoni, waandishi wakaanza kunipigia na mimi nikaamua kuzungumza na wenzangu kupata uhakika. Kila mmoja hakuwa akilijua hili. Sitaki kuzika kichwa changu kwenye mchanga, yaani nifiche au niseme tu. Nafikiri Okwi hadi sasa hayuko kwenye mipango yetu.

Na tuangalie, haiwezi ikawa kila siku tunarudi kwa mtu yuleyule. Halafu lazima mjue, sisi tutafanya kazi ya usajili kutokana na ripoti ya mwalimu inasemaje. Ikitokea anatakiwa pia mtajua lakini itakuwa kutoka kwetu.

SALEHJEMBE:  Kwa kuwa mwalimu ameshakabidhi ripoti, labda mnatakiwa kuongeza wachezaji katika nafasi zipi?
Hans Poppe: Nani kakuambia amekabidhi?

SALEHJEMBE:  Uhakika upo, labda tueleze tu, mwalimu anataka nini?
Hans Poppe:  Kesho (leo) tutakutana kamati ya utendaji na kuijadili ripoti yake. Najua tunatakiwa kuongeza kipa, beki na mshambuliaji mmoja. Hivyo sasa siwezi kuzungumzia sana.

SALEHJEMBE: Mkude na Zimbwe au Tshabalala, vipi hawa maana mmekaa kimya na Yanga wanaonekana kutupa ndoano, mko tayari waende?
Hans Poppe: Mimi nashangazwa sana na hawa watu wanaosema wanakwenda sijui wapi, tena hawa watu bado wana mkataba na sisi.

SALEHJEMBE:  Lakini unakwenda ukingoni?
Hans Poppe: Mimi nimeshazungumza nao na kila upande mazungumzo mazuri kabisa hadi sasa na upande mwingine naweza kusema tumemalizana. Naweza kukuhakikishia kwamba hao watabaki Simba.

SALEHJEMBE:  Watabaki vipi wakati umesema bado upande hamjamaliza makubaliano?
Hans Poppe: Kweli, lakini tunavyokwenda hatuna shida ya kusema tutashindwana. Lengo ni kumaliza hili na kuendelea pamoja. Ila kama itaonekana kuna sehemu imeshindikana, basi mtajua imekuwaje.

SALEHJEMBE: Nini unaona mnatakiwa kufanya ili kumaliza ligi na ubingwa?
Hans Poppe: Kwanza umoja, malengo yanayofanana kwamba tunataka ubingwa. Mapenzi ya dhati kwa timu na klabu na kila mmoja awe kweli kwa ajili ya kuitumikia Simba na kuipa manufaa.

SALEHJEMBE: Sawa, kila la kheri.

Hans Poppe: Ahsante.

2 COMMENTS:

 1. Waandishi wetu wailo wengi huandika kwa mazoea, kwani ni lazima kuandika habari za spot? mara Okwi na Kipre haooo Simba!!! sasa leo M/kiti wa Usajiri anawajibu hatukuwa na mpango na Okwi ila wakimuhitaji tutawaambia, waandishi msifanye kazi na mashabiki wanaohisi usajili kwa maneno ya ulaiani, mara mkude anakuja yanga, aje huku kufanya nini?
  poleni

  ReplyDelete
  Replies
  1. hongera hujajib kwa hisia😁😁😁

   Delete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV