November 14, 2016




Na Saleh Ally
MWAKA 2010 nilibahatika kumuona Mesut Ozil akiichezea Werder Bremen kwenye uwanja wao wa nyumbani. Nikahoji kuhusiana na mchezaji huyo, kwamba vipi hayuko klabu kubwa kama Bayern Munich?

Mwenyeji wetu uwanjani pale akasema, mjadala wa viongozi wa Werder Bremen
 ni kuwa Ozil ni kati ya wachezaji wanaopewa nafasi kubwa ya kufika mbali na anachukuliwa kama sehemu ya mradi katika klabu hiyo na wanaamini baada ya muda atakwenda Bayern Munich au klabu kubwa za Hispania na England.

Akanifafanulia mimi na Mtanzania mwingine ambaye tulikuwa pale uwanjani mjini Bremen, Ujerumani kwamba kinachoweza kumkwamisha Ozil ni misimamo, hasa ile ya kidini kwa kuwa wakati mwingine anakataa kufanya mambo kadhaa kwa kuwa Uislamu unakataza.

Mimi ilinishangaza, sikuamini mtu anaweza kukwama kwa kufuata misingi ya dini na hata nilipomueleza, mjadala ulikuwa mrefu bila sababu za msingi, nikaamua kuacha.

Miezi michache baadaye Ozil mwenye asili ya Uturuki, aliondoka Bremen na kujiunga na Real Madrid. Nikapata nafasi ya kuwasiliana na rafiki yangu huyo ambaye aliniambia kwa soka atafika mbali, bado anaamini hivyo ila kwa ile misimamo yake atafeli. Bado Ozil akafanya vizuri na Real Madrid, tena sana.


Ilipofikia anaondoka kwenda Arsenal, rafiki yangu alikuwa wa kwanza kunipigia na kuniambia anaondoka kwenda London kutoka jijini Madrid, kwake aliona kama anafeli na kocha alikuwa hajafurahishwa na misimamo yake, kwa kifupi alidai ni mtukutu wa chinichini.

Nikamueleza alikuwa akienda Arsenal kwa bei kubwa ya pauni milioni 42.5 ambayo ni rekodi kwa Arsenal, ukaanza tena mjadala mrefu usio na faida. Nikaamua kuachana nao.

Tangu ametua Arsenal, Ozil ni staa na tegemeo katika kikosi hicho cha Arsene Wenger. Asipofunga anatoa pasi ya bao na amekuwa gumzo kwa pasi zake ndani ya England.

Jicho la Wenger linastahili pongezi kwa kuwa kamnunua mchezaji wake wa kwanza kwa bei ghali licha ya kupewa sifa ya ubahili, kweli imeonekana alilenga na alichofanya ni sahihi.


Baada ya Kocha Jose Mourinho aliyewahi kumfananisha Ozil na Zinedine Zidane kutokana na pasi zake kuonyesha nia yake ya kumsajili atue Man United, nami nikampigia simu rafiki yangu wa Ujerumani na kumkumbusha namna ambavyo Ozil anavyozidi kupaa akipitia misimamo yake. Ukaanza ule mjadala mrefu ambao umejaa ubishi usio na msingi, nikauacha tena.

Pamoja na kuuacha mjadala huo, kwangu nimejifunza kwamba ni vizuri binadamu kuwa na misimamo yako, kuishi unavyotaka ilimradi unakuwa na nidhamu na kazi yako, pia unawaheshimu watu waliokuzunguka na wengine wote inapobidi.

Ozil amekuwa akizungumza namna anavyofanya. Katika kila mechi husali mara sita. Kipindi cha kwanza, kabla ya kuingia, akiwa na wenzake na wakati akitoka na kipindi cha pili hivyohivyo.

Amewahi kuzungumzia suala la kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kwamba kuna wakati huwa hafungi kwa kuwa analazimika kula na kunywa maji mengi kulingana na hali halisi, lakini bado kuna baadhi ya mechi hucheza akiwa amefunga.


Ozil ni kati ya wachezaji wanaoendesha magari makali ya bei ghali, kati ya wachezaji wachache kabisa wenye nyumba kali na ghali. Zile anazoishi au alizonunua, zote ni nyumba hasa.

Hata mpenzi, amechagua mrembo hasa na ukimuona utasema naam! Huyu ni mtu anayefanya mambo yake anavyotaka yeye, anaishi anavyotaka yeye lakini kazi yake inaonekana ni bora kila anapokwenda.

Katika sehemu alizopita hasa katika suala la utoaji pasi, Ozil alikuwa mwanasoka bora kwa utoaji pasi zinazozaa mabao Ulaya yote, hii ilikuwa ni msimu wa 2010-11. Jiulize watu kama Andres Iniesta na Xavi Hernandez walikuwa wapi na aliwazidi vipi, jibu ni kwamba ana kipaji na anajituma kwa sababu anaithamini kazi yake.

Msimu wa 2011-12, Ozil alikuwa ndiye namba moja katika utoaji pasi hizo za mabao maarufu kama asisti mbele ya Xavi ambaye aliaminika ni pass master wa La Liga. Hiki si kitu kidogo.


Katika Kombe la Dunia mwaka 2010 ambako Ujerumani ilishika nafasi ya tatu na Hispania kulibeba ikiifunga Uholanzi kwa bao la Iniesta, yeye ndiye alikuwa mtoa pasi bora na nyingi zilizozaa mabao.

Alipotua Arsenal, hilo tena limejirejesha na ameonyesha hii kazi ya utoaji wa pasi za mabao si kazi anayoibahatisha na Mourinho hakukosea kumfananisha na Zidane.

Leo anamhitaji, inaonyesha wazi kabisa kwamba Mourinho amegundua anakosa mtoaji wa pasi za mabao kwa kuwa watu wa kumalizia anao wa uhakika lakini hawana fundi nyuma yao.


Hauwezi tena ukakataa kuwa Ozil ndiye staa wa England kwa kipindi hiki kwa maana ya ubora wa kazi, wengine watamfuatia.

Licha ya kuwa si mwenye mambo mengi nje ya uwanja, Machi mwaka huu alifikisha mashabiki milioni 28 kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook na kushika nafasi ya saba baada ya Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, David Beckham, Neymar, Kaka na Ronaldinho, wengi wakiwa wamejichimbia mizizi tokea awali.

Kupitia Ozil unaweza kujifunza mengi, mfano kumuachia mtu aishi maisha yake na kuikubali kazi yake. Pili kuishi unavyotaka lakini ukafanya kazi yako kwa ubora wa juu. Ozil anaonekana anaipenda kazi yake na anajituma, ndiyo maana hachuji.

Pia si mtu wa kukata tamaa, hata baada ya kuondoka Madrid, alipotua Arsenal ‘hakufa’ ameendelea kufanya yake na huenda akang’ara zaidi. Ntaona kama nina muda, nitampigia tena yule rafiki yangu wa Ujerumani, nikiona mjadala mrefu bila sababu za msingi, nitaacha naye tena!

SOURCE: CHAMPIONI



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic