November 12, 2016



Na Saleh Ally
MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu Bara umeisha mechi 240 zikiwa zimepigwa.

Simba ndiyo vinara, wanafuatiwa na watani wao wa jadi, Yanga, ambao ndiyo mabingwa watetezi wa ligi hiyo kwa misimu miwili mfululizo.

Wakati mzunguko unaisha, inaonyesha hivi, hadi mechi ya 13 kwa kila timu, Simba ilikuwa inaongoza kwa tofauti ya pointi nane.

Kama ingeshinda mechi zote mbili za mwisho dhidi ya African Lyon na Prisons ya Mbeya, basi ingerudi kuanza mzunguko wa pili ikiwa na pointi nane za uongozi, jambo ambalo lingekuwa linawapa nafasi nzuri ya kujipanga na ubingwa.

 Lakini sasa, mambo ni tofauti kabisa kwa kuwa kama watarejea, pointi mbili maana yake ni kupoteza mechi moja na kutoa nafasi moja ya ushindi kwa mwingine kupanda juu.
Mzunguko huo wa kwanza, umetoa funzo katika mambo kadhaa katika timu mbalimbali ambazo zinaonyesha ukomavu, papara, ukosefu wa subira na wakati mwingine uchanga wa utendaji katika maamuzi sahihi na yasiyo sahihi.


 Lakini imeonekana kiasi gani papara imesababisha mambo kadhaa kutokwenda vizuri na hata timu kuanza kuyumba na hii huenda ikawa dawa au sumu katika mzunguko wa pili katika timu nyingine, raha ni kwamba kila upande unaweza kuchagua mwenyewe, unataka upande mzuri au upande mbovu.

Timu nne ninaweza kuzizungumzia katika wigo ambao nimeamua kutaka kuutanua ili kujifunza ni Yanga, Simba, Azam FC na Stand United.


Azam FC:
Ilianza kwa kusuasua sana, ilikwenda na kufikia kupoteza mechi nne. Kwa tafsiri ya kawaida ikawa ni kibonde na ikaonekana mambo yao ni magumu kabisa.
Gumzo likawa ni kutimuliwa kwa kocha kijana, Zeben Hernandez kwamba mfumo wa Kihispania hauna njia ya ‘kutusua’ katika soka nchini.

Uongozi wa Azam FC, safari hii ukaonyesha ukomavu na mambo ambayo zamani haukuwa ukifanya. Maana ulichofanya ni kuendelea kuwaamini na kuwasapoti makocha wake na hii ilikuwa ni baada ya tathmini nzuri ya kuona tatizo si makocha pekee lakini mabadiliko ya kuwakosa wachezaji kadhaa kama Kipre Tchetche, Farid Mussa na kadhalika, yaliwaathiri.

Mwisho Azam FC wamefanikiwa kurejea kwenye reli kutoka nafasi ya saba, sita na sasa wako nafasi ya tatu, wanakwenda kupumzika, watajipanga kwa usajili na maandalizi bora, wakirejea, kazi ipo.


Stand United:
Ndiyo timu kutoka nje ya Dar es Salaam iliyoongoza ligi muda mrefu, ilikaa nafasi ya pili muda mrefu na  hii ilionekana Patrick Liewig, Mfaransa huyu mkongwe alikuwa amezoea mipango na sasa alianza kusonga kwa kasi.

Yanga, Azam FC wakapokea vipigo. Lakini mwisho uongozi ukaona aondoke, kisa ni fedha na hakukuwa na tathmini au busara sahihi ambayo ingetumika kuhakikisha kocha huyo anaendelea kubaki angalau amalize mzunguko wa kwanza na kama lingekuwa ni suala la gharama, wangeanza kujipanga wakati wa maandalizi ya mzunguko wa pili.
Wakaacha aondoke, sasa mzunguko wa kwanza unaisha wako katika nafasi ya sita, mechi tatu wamezipoteza ndani ya mechi sita walizocheza wakiwa chini ya kocha msaidizi Athumani Bilal ‘Bilo’.
 Kamwe simdharau Bilo, lakini utaalamu wake bado hauwezi kufanana na ule wa Liewig, pia alihitaji muda wa maandalizi akiwa mwenyewe. Papara za watu wa Stand wakiona kila kitu kinawezekana, unaona sasa, nafasi ya sita ni tatizo na wasipojipanga vema, mzunguko wa pili wanaweza kuwa na hali mbaya zaidi.

Yanga:
Huenda wamezidi kuonyesha ukomavu. Utaona ndani ya mechi kumi walishapoteza mbili, tena uongozi wao ukiwa katika mtikisiko mkubwa kuhusiana na suala la mabadiliko lakini ikaonekana kuna wachache wanapinga na inaonekana nyuma yao kuna wenye madaraka, wenye uwezo kuamua, hivyo uongozi haukuwa umetulia.

Lakini bado mwisho, unaona baada ya kupoteza mechi mbili, wamejipanga na kujadili nini cha kufanya, wamerudi kwenye msitari. Wamemaliza mzunguko wa kwanza wakiwa na tofauti ya pointi mbili tu na vinara wa ligi hiyo Simba ambao wamekuwa wanateleza na ‘ganda la ndizi’ kurejea nyuma.

Yanga imepitia migogoro mingi wakati wa mzunguko wa kwanza. Lakini mwisho wanaonyesha kama watakuwa wametulia, basi mzunguko wa pili itakuwa kazi ngumu kuwazuia na hasa kama Kocha George Lwandamina atakuwa ameweza kupanga mambo yake sawa na kufanya vema.

Simba:
Hii ni timu ya mwisho ambayo imetoa funzo, kwani hadi mechi ya 13 walikuwa wanaongoza kwa tofauti ya pointi nane, hadi mechi ya 15 wanaongoza kwa tofauti ya pointi mbili tu!

Unaweza kuona ni kama miujiza, lakini kukosekana kwa utulivu, busara na viongozi ambao wana sauti na uwezo wa kuamua sahihi ndiyo kimewaangusha Simba.

Angalia baada ya kufungwa na Lyon, ikawa lawama, maneno, ukali, kila mmoja akiona mwenzake amekosea. Wamesafiri kwenda Mbeya, nako wamepoteza.
Utasikia vurugu zimeanza kimyakimya, wapo waliotangaza kujiuzulu, wapo wanaopinga na hawafurahii. Basi ni tafrani tu.

Ndani ya Simba kila mmoja ni bosi, kila mmoja ana uwezo wa kuamua au kupinga la mwingine. Hii itaendelea kuwaangusha na imekuwa sehemu ya anguko la Simba kwa misimu miwili mfululizo.

Simba hakuna asiyejua, hili ni tatizo jingine. Na hawana ujanja, lazima wajipange hasa wakati wa mzunguko wa pili na wasipofanya hivyo, mzunguko wa pili unaweza kuisha wakiwa katika nafasi ya tatu ambayo wamekuwa wakiitumikia kwa zaidi ya misimu miwili sasa.


Mzunguko wa kwanza, umeacha funzo na kwa wale ambao watakuwa tayari kubadilika na kujifunza kupitia hayo makosa, watafanikiwa lakini wakishindwa, watakuwa na anguko la mshituko zaidi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic