PLUIJM |
Nahodha wa Yanga, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, ametoa neno la heshima kwa kocha wao anayeondoka, Hans van Der Pluijm, raia wa Uholanzi, kwa kusema anapaswa kupewa heshima zote kwa jinsi alivyowaongoza katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.
Niyonzima ameyasema hayo siku chache baada ya Yanga kumpa mkataba wa miaka miwili, Mzambia, George Lwandamina ambaye anachukua mikoba ya Mholanzi huyo, ingawa uongozi unawazunga wanachama kwa kukana.
NIYONZIMA |
Mnyarwanda huyo amesema ugumu walioupitia katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo, bila ya uwepo wa Pluijm hajui kama wangefanikiwa kuwa nafasi ya pili waliyopo sasa nyuma ya Simba.
“Haikuwa rahisi kwa sisi kumaliza mzunguko huu tukiwa hapa kwani hakuna aliyetarajia kama tungeweza kupambana kwa jinsi tulivyokuwa tumechoka, lakini tunamshukuru Mungu kwa kutupigania.
“Yaani kama asingekuwa Pluijm na benchi zima la ufundi kwa jinsi walivyokuwa wakitupa moyo wa kupambana na kutuambia tusikate tamaa, sidhani kama tungefanikiwa.
“Niseme tu, nimeamini kwamba katika dunia hii lolote linawezekana, hivyo tunaamini kwamba mzunguko wa pili tutafanya vizuri zaidi ya hapa,” alisema Niyonzima.
Yanga imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa nafasi ya pili baada ya kujikusanyia pointi 33, nyuma ya vinara Simba wanaoongoza ligi hiyo kwa pointi 35.
Hata hivyo, Niyonzima alisema kuondoka kwa Pluijm na kuja Lwandamina wao kama wachezaji hawana la kusema zaidi ya kuendelea kushirikiana naye ili tu kuubakisha ubingwa Yanga kwa mara ya tatu mfululizo kwani hakuna timu itakayozuia hilo.
"Tutafanya kazi na kocha yeyote yule atakayekuja, lakini kwa sasa niseme tu Simba wapo kwenye nafasi yetu na hilo linajulikana, wao wamekaa tu pale kwa muda, mzunguko wa pili lazima watuachie na tuwe mabingwa. Mzunguko wa pili uwezo wetu utaongezeka maradufu na tutacheza kufa na kupona,” alisema Niyonzima.
SOURCE: CHAMPIONI
(LIKO MTAANI LEO)
0 COMMENTS:
Post a Comment