November 5, 2016
Na Saleh Ally
ALEX Chapman Ferguson hakuwahi kuwa na ndoto ya kuinoa Manchester United. Wakati akijiandaa kutoka Aberdeen na kwenda England kufanya kazi ya ukocha, lengo lake lilikuwa ni Liverpool FC.

Liverpool ndiyo ilikuwa ndiyo yenye jina kubwa zaidi, ikashindikana baada ya wao kumdanganya na kumchukua kocha mwingine. Hata alipoajiriwa Manchester United mwaka 1986, aliapa siku moja angeiangusha Liverpool, hakuna aliyeamini.

Baada ya miaka 27 kazini Manchester United, aliamua kustaafu huku akiwa ametimiza lengo lake; Manchester United imekuwa kubwa zaidi ya Liverpool na mchango wake umesaidia kwa zaidi ya asilimia 60.

Lakini ni vizuri kujua kwa nini alisaidia kwa kuwa misimu ya mwanzo kwake haikuwa mizuri na presha ilikuwa kubwa kupindukia, lakini alivumilia, akavuka na mwisho akageuka na kuwa kocha gumzo kuliko mwingine katika ngazi ya klabu kwa kipindi kirefu cha zaidi ya miaka 20.


Msimu wa kwanza, Man United ilishika nafasi ya 11, msimu uliofuata wa 1987-88 ikawa ya pili, halafu 1988-89 ikaporomoka hadi nafasi ya 11.

Ikionekana kuwa msimu wa 1989-90 ingekuwa na maboresho baada ya usajili, Man United ikashika nafasi ya tatu na uongozi wa Man United chini ya Edward Martin uliendelea kumshikilia Ferguson ukisema unamuamini na atabadilika.

Mabadiliko ya Ferguson yalianza msimu wa 1990-91 aliposhika nafasi ya sita, halafu 1991-92 akatwaa nafasi ya pili, kasi ikaanza.

Msimu wa 1992-94, baraka ikaanza kwa Man United kubeba ubingwa na msimu uliofuata ikafanya hivyo tena. Ferguson akawa ameshika kasi na chini ya uongozi wake tangu 1991-92 waliposhika nafasi ya pili chini yake, hawakuwahi tena kuteremka chini ya nafasi ya tatu kwa misimu 12 hadi alipostaafu akiwa amebeba makombe ya ubingwa wa England 13.


Kabla mambo hayajakaa sawa, misimu mitano ya mwanzo ya Ferguson ilikuwa migumu zaidi ya ile mingine 22 na wengi walimpachika jina la muuza baa kwa kuwa alikuwa akimiliki baa kwao Govan, Scotland akiwa anatokea familia ya wagonga vyuma ambao kazi yao ilikuwa ni kutengeneza meli.

Akiwa na Manchester United alishinda mechi 894, sare 337, akapoteza 267 lakini mwisho amestaafu akiwa shujaa wa klabu hiyo.

Leo ndani ya misimu minne tayari Man United imeajiri makocha watatu maarufu au mahiri lakini hakuna anayeonekana kuwa na uwezo wa kuvaa viatu vyake licha ya fedha nyingi za usajili.

David Moyes ambaye aliifundisha hakumaliza hata msimu akiwa ametumia pauni milioni 64.6 (Sh bilioni 170), akaonekana hafai, akatimuliwa na nafasi yake ikachukuliwa na Louis van Gaal huyu ni kocha mkongwe na maarufu duniani, aliwahi kuzinoa Ajax, Barcelona na Bayern Munich kwa mafanikio makubwa, lakini mambo yakamshinda.

Van Gaal alitumia zaidi ya pauni milioni 261.7 (zaidi ya Sh bilioni 692). Akajitahidi akabeba Kombe la FA, bado akaonekana hafai na Man United wakamwaga na kumchukua mwanafunzi wake, Jose Mourinho ambaye anaaminika lakini naye inaonekana mambo ni magumu.

Mourinho na ubora wake amekuwa akipokea vipigo mara kwa mara, jambo ambalo linawakatisha tamaa Man United wengi, wakiwemo mashabiki wake kibao walio Tanzania.


Inawezekana kabisa, Man United wakawa wamejifunza kwamba walikosea kumuondoa Moyes, halafu wakafanya haraka kumfukuza Van Gaal na haitakuwa vizuri kumuondoa Mourinho kwa sasa.

Huenda wamelazimika misimu miwili ya Moyes na Van Gaal kuiona migumu kwa kuwa wana haraka. Angalia hata walipotwaa ubingwa wa FA wakaona nao ni mdogo.

Kocha aliyekaa muda mchache Van Gaal, akabeba Kombe la FA ambalo wengine wanalisumbukia kwa zaidi ya miaka 15, bado alikuwa vizuri sana.

Viatu vya Ferguson havivaliwi kirahisi. Maana hata yeye wakati anaanza kuvivaa alisumbuka sana. Vilipomtosha akaanza kupiga mwendo na kutimua vumbi. Kizazi cha kuanzia miaka ya 2000 wengi wanapenda Man United lakini mtu maarufu kuliko wengine kwao alikuwa ni Ferguson.

Mbaya zaidi, asilimia zaidi ya 57 ya mashabiki hao, hawakuwa mashabiki wa Man United wakati Ferguson akisumbuka kuvivaa vizuri viatu ambavyo alivikuta na vilikuwa havimtoshi.

Mashabiki wa Man United walimshangaa Moyes kuganda na kumaliza katika nafasi ya saba, wakasahau Ferguson ambaye ni shujaa wao alishika hadi nafasi ya 13, alishika nafasi ya 11 mara mbili. Baadaye ndiyo akakaa sawa.


Mourinho anahitaji msimu mmoja wa kutofanya vizuri kwa kiwango cha juu, msimu unaofuata atakuwa na uwezo wa kubadili timu na kama kweli mashabiki wanahitaji Man United mpya, lazima walikubali hilo la sivyo, zoezi la kujaribia viatu vya Ferguson litaendelea bila kwisha huku makombe yakiendelea kukauka Old Trafford.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV