November 12, 2016Simba imeishtukia kasi ya Yanga katika Ligi Kuu Bara huku yenyewe ikiteleza hivyo klabu hiyo imepanga kuweka kambi ya muda mfupi nchini Ethiopia kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.

Licha ya kuongoza ligi ikiwa na pointi 35, Simba ilimaliza mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo kwa kusuasua baada ya kufungwa mechi mbili mfululizo na African Lyon kisha Prisons na kuzua hofu kwa mashabiki.

Kocha wa Simba, Joseph Omog raia wa Cameroon ametoa ruhusa ya mapumziko kwa wachezaji wake kwa muda wa wiki mbili tu kuanzia jana na Novemba 28, mwaka huu wataanza kambi kujiandaa na mzunguko wa pili.

“Nimetoa likizo ya wiki mbili na Novemba 28, tutaanza rasmi maandalizi ya raundi ya pili. Nimefanya hivyo kwa kutaka tuwe na maandalizi ya kutosha na kuhakikisha tunarekebisha makosa tuliyofanya kwenye mechi za mwisho.

“Nimepanga tupate kambi ya nje ya nchi ambayo itakuwa tulivu na kupata mechi mbili au tatu za kujipima nguvu.
“Ligi ni ngumu na ninajua Yanga wamefanya vizuri sasa ili tupambane nao vizuri ni lazima tuweka kambi hiyo kwani naamini tukipata utulivu tutafanya vizuri tukianza ligi,” alisema Omog.

Katika hatua nyingine, Mratibu wa Simba, Abbas Ally ‘Gazza’ alilithibitishia Championi Jumamosi kuwa, wataweka kambi nchini Ethiopia ambako wamepata mualiko maalum, mbali na mazoezi pia watacheza mechi kadhaa za kirafiki.

Mzunguko wa pili wa ligi kuu unatarajiwa kuanza Desemba 17, mwaka huu lakini Omog amesisitiza kukiimarisha zaidi kikosi chake ili kuepuka presha ya Yanga katika kuwania ubingwa.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV